Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum
Felister Mdemu amewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii mkoa wa Rukwa kuzitumia
pikipiki waliokabidhiwa ili kuleta ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mdemu
ameyasema hayo jana Oktoba 24, 2025 wakati akikabidhi pikipiki 8 kwa Maafisa
Maendeleo ya Jamii kutoka Halmashauri za Mkoa wa Rukwa.
Amesema
Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi
Maalum inakabidhi pikipiki nane (8) kwa Halmashauri nne za Mkoa wa Rukwa kwa
ajili ya Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Kata hatua inayolenga kuwawezesha
maafisa hao kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi katika kuwahudumia
wananchi.
Mdemu
amebainisha kuwa pikipiki hizo ni nyenzo muhimu za kazi zitakazorahisisha
mawasiliano na ufuatiliaji wa shughuli za maendeleo katika maeneo ya vijijini
na Kata. Amesema kuwa Serikali imekusudia kuongeza ufanisi wa Maafisa Maendeleo
ya Jamii katika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala ya maendeleo, kuimarisha
ushiriki wa jamii katika miradi ya kijamii, na kuchochea uwajibikaji katika
ngazi za chini za utawala.
Naye
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Daudi Sebyiga, amepongeza hatua
hiyo akieleza kuwa itaboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wa sekta ya
maendeleo ya jamii katika Halmashauri za Mkoa wa Rukwa huku akisisitiza kuwa
pikipiki hizo zitaongeza kasi ya utoaji huduma na kufikisha elimu ya maendeleo
kwa wananchi kwa wakati.
Nao
Maafisa Maendeleo ya Jamii waliopokea pikipiki hizo wameishukuru Serikali ya
kwa kuwapatia vyombo hivyo vya usafiri, wakibainisha kuwa vitasaidia kupunguza
changamoto ya usafiri na kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao katika maeneo
ya vijijini.



0 Maoni