Timu
ya Kilimanjaro FF inayomilikiwa na kuendeshwa na Watanzania waishio nchini
Sweden imeshika nafasi ya tatu katika ligi ya daraja la sita kwenye jiji la
Stockholm katika msimu wa 2024/25 iliyohitimishwa mwezi Oktoba.
Akimtaarifu
Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mhe. Mobhare Matinyi, wakati wa hafla fupi
nyumbani kwa balozi ya kulikabidhi kombe la ushindi wa Bonanza la Serengeti,
Mwenyekiti wa Kilimanjaro, Norman Jasson, alisema mwakani wamepania kushika
nafasi ya kwanza au ya pili ili waingie daraja la tano.
Mhe.
Balozi Matinyi aliwapongeza wachezaji wa Kilimanjaro na kuwataarifu kwamba Ubalozi
unaitafutia wadhamini kutoka nyumbani Tanzania ili mbali ya kucheza soka, timu
hiyo pia ilitangaze vema jina la Tanzania na fursa zilizopo nchini katika
uwekezaji, biashara na utalii.
Vilevile,
Mhe. Balozi Matinyi aliwaambia wachezaji na uongozi wa Kilimanjaro kwamba
mipango inaendelea kwa kushirikiana na mamlaka za michezo nchini ili
ikifanikiwa basi wachezaji vijana wa Tanzania waje nchini Sweden kuiongezea
nguvu Kilimanjaro na pia kuwapa uzoefu wa kucheza Ulaya na pengine kubakia
katika timu za Ulaya.
Kwa
mwaka huu timu za Stocksunds IF na IFK Lidingö BK ndizo zimeshika nafasi za juu
na hivyo kupanda daraja. Mfumo wa michuano ya soka nchini Sweden una madaraja
saba kuanzia ngazi za miji.
Katika
hafla hiyo iliyofanyika kabla ya tukio la kuangalia mechi ya Yanga na Silver
Striker kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, nahodha wa
Kilimanjaro, Richard Ntirugererwa, maarufu kama Messy, alimkabidhi Mhe. Balozi
kombe la Bonanza la Serengeti ambalo ililitwaa mwezi Agosti nchini Ubelgiji kwa
mara ya nne mfululizo.
Timu
ya Kilimanjaro leo Jumapili tarehe 26 Oktoba, 2025, inaendelea na raundi ya
pili ya michuano ya mtoano ya Kombe la Stockholm ambapo mshindi wake atashiriki
kwenye michuano ya Chama cha Soka cha Sweden (SFF).
Ubalozi
wa Tanzania, Stockholm, Sweden.
Jumapili,
Oktoba 26, 2025.

0 Maoni