KENYA YATUPA SOMO LA MAUMIVU: Tanzania Inatakiwa Kushtuka – Amani Si Bahati Nasibu!

 

Kwa takribani miaka miwili, Kenya, jirani yetu wa karibu, imekuwa uwanja wa majaribio ya vurugu. Maandamano ya mara kwa mara yameacha vifo, majeraha, na uharibifu mkubwa wa mali. Hali hii haikutikisa tu uchumi, bali iliyumbisha kabisa utulivu wa kijamii na huo ndio msingi wa funzo letu.

Dkt. Daniel Mwaisaka, mchambuzi wa siasa za Afrika Mashariki kutoka Chuo Kikuu cha Bugema, anatoa angalizo la moja kwa moja:

“Kenya ilianza kwa madai ya kisiasa, lakini yakageuka vurugu ya wazi. Uwekezaji uliporomoka ghafla, bei za bidhaa zikapanda kwa kasi, na walioumia zaidi ni wananchi wa kawaida.”

Vurugu hizi ziliiacha Nairobi ikiwa imejeruhiwa. Sekta ya utalii iliporomoka kwa zaidi ya asilimia 40, biashara nyingi zikifungwa, na maelfu ya vijana wakipoteza ajira zao kutokana na hofu ya usalama.

Ushuhuda wa Maumivu: Kura Ni Silaha Bora Kuliko Jiwe

Sauti za walioathirika nazo zinatoa ushahidi usioweza kupingwa. Bi. Amina Yusuf, mfanyabiashara wa soko la Gikomba, anasimulia kwa uchungu wa moyo: "Tulipoteza kila kitu. Maduka yaliibwa, majirani wakagawanyika kisiasa. Tulijifunza kuwa amani ni bora kuliko vurugu.”

Vilevile, Brian Otieno, kijana wa teknolojia kutoka Kenya, anakiri kwa masikitiko: “Nilidhani maandamano yangeleta mabadiliko, lakini sasa naona tulitumiwa kisiasa. Rafiki zangu wawili walipoteza maisha. Sasa naamini kura ni silaha bora kuliko jiwe.”

Kauli hizi za Brian na Amina zinapaswa kuingia akilini mwa kila Mtanzania anayechezea wazo la ghasia.

Wito wa Hekima: Tanzania Si Mahali pa Kujaribu Moto

Wakati maneno ya uchochezi yakizidi kujaa mitandaoni, viongozi wa kiroho na wazee wanarejea kwenye hekima. Askofu Emmanuel wa Kanisa la Wokovu Arusha anatukumbusha: “Watanzania hawapaswi kuruhusu siasa za chuki wala kugawanyika. Maandamano hayajengi taifa, yanabomoa mshikamano.”

Naye Mzee Juma Kihampa kutoka Morogoro anawasihi wazazi: “Tuwafundishe vijana kuwa kura ni silaha salama ya mabadiliko, si mawe wala moto. Tuwalee kwenye misingi ya amani na subira.”

Tanzania imetambulika kimataifa kama "kisiwa cha amani", na urithi huu ni tunu yetu isiyoweza kuwekwa rehani. Wachambuzi wa siasa wanakubaliana: Wanasiasa wana wajibu wa kuhimiza vijana kujenga badala ya kubomoa.

Kila Mtanzania anapaswa kuwa mlinzi wa amani, kukataa kabisa siasa za chuki, na kutumia sanduku la kura kama njia pekee halali ya kutafuta mabadiliko. Tujifunze kutoka kwa Kenya: Vurugu havileti maendeleo huharibu maisha. Amani ndiyo mama wa maendeleo, tuilinde kwa vizazi vijavyo!

Chapisha Maoni

0 Maoni