AWF yaikabidhi TAWA jengo la kikosi cha mbwa nusa

 

Shirika la Kimataifa la African Wildlife Foundation (AWF) imeikabidhi rasmi Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) majengo maalum kwa ajili ya Kikosi cha Mbwa Nusa (TAWA K9-UNIT) kwa lengo la kuimarisha ulinzi wa rasilimali ya wanyamapori katika maeneo ya Mipakani mwa Nchi, Vituo vya Ushuru wa Forodha na Viwanja vya Ndege vya Kilimanjaro na Arusha.

Akizungumza jana katika hafla ya uzinduzi na makabidhiano ya jengo la Kikosi cha Mbwa Nusa zilizofanyika katika Ofisi za TAWA, Kanda ya Kaskazini zilizopo jijini Arusha, Mgeni Rasmi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA, Mej.Jen (Mstaafu) Hamis Semfuko amesema Kikosi cha mbwa nusa (Sniffing dogs) ni nyenzo muhimu ambayo imekuwa ni msaada katika kudhibiti uhalifu unaohusiana na usafirishaji haramu wa nyara za Serikali na biashara haramu ya wanyamapori.

“Kikosi hiki kimekuwa msaada mkubwa hasa katika kudhibiti utoroshaji nyara kupitia mipakani, vituo vya usafirishaji na forodha,” amesema Semfuko.

Mej.Jen (Mstaafu) Semfuko ameongeza kuwa TAWA itaendelea kukiimarisha Kikosi hiki kwa kuongeza idadi ya watumishi katika kikosi, kuongeza vitendea kazi pamoja na kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa watumishi wa kikosi cha Mbwa Nusa.

Sambamba na hilo, Mej.Jen (Mstaafu) Semfuko amewashukuru AWF kwa mchango wao uliowezesha ujenzi wa jengo la (TAWA-K9 UNIT). Aidha, ametoa rai kwa wadau wengine wa Uhifadhi kuendelea kushirikana na TAWA katika kuimarisha ulinzi wa rasilimali ya wanyamapori.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la AWF, Pastory Magingi, amesema Jengo hili limekabidhiwa kwa ajili ya kuimarisha utekelezaji wa sheria kupitia mbwa waliopatiwa mafunzo, sambamba na kuwapatia mbwa hawa makazi ya kudumu.

Pamoja na hilo, Bw. Magingi ameongeza kuwa AWF kwa kushirikiana na TAWA imeweza kuandaa miongozo mbalimbali kwa ajili ya uendeshaji wa vikosi vya mbwa wa uhifadhi.

Awali, akitoa salamu za ukaribisho, Kaimu Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA, Mlage Yussuf Kabange amesema mashirikiano mazuri yaliyopo baina ya TAWA na AWF yameweza kufanikisha ujenzi wa jengo hilo ambalo linajumuisha vyumba sita (6) vya mbwa, Ofisi, Stoo ya chakula, maliwato na eneo la wazi lenye uzio kwa ajili ya mazoezi ya mbwa.

Vilevile, Kamishna Kabange ameongeza kuwa pamoja na Mbwa Nusa (Sniffing dogs), TAWA imepanga kuanzisha Kikosi cha Mbwa wa ufuatiliaji (Tracking dogs) na kuanzisha Kituo cha mafunzo ya Mbwa (Dog Training Centre).

Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi TAWA, Segoline Tarimo ambaye alimwakilisha Kamanda wa Kanda ya Kaskazini amesema tangu kuanzishwa kwa Kikosi cha Mbwa, Kikosi kimepata mafanikio mengi ikiwemo kudhibiti uhalifu wa utoroshaji wa nyara kupitia kiwanja cha KIA na maeneo ya mipakani.

Kadhalika, ameongeza kuwa majengo haya yaliyokabidhiwa yatawezesha kikosi kufanya kazi katika mazingira bora na kwa ufanisi zaidi.

Hafla hii ya makabidhiano ya Jengo la Kikosi cha Mbwa Nusa, iliambatana na kusaini makubaliano (Memorandum of Understanding) baina ya AWF na TAWA.  Makubaliano hayo yalijikita katika matumizi ya Mbwa Nusa na matumizi ya teknolojia katika kudhibiti uhalifu wa nyara za wanyamapori.


           Na. Joyce Ndunguru - Arusha

Chapisha Maoni

0 Maoni