Chama Cha
Mapinduzi CCM kimeahidi kuendelea kuimarisha huduma za kinga ndani ya jamii
kupitia program kabambe ya Wahudumu wa Afya ngazi ya jamii ambao wamewezeshwa
kwa mafunzo na kupewa vifaa kwa ajili ya kutoa huduma za msingi za afya pamoja
na elimu ya afya ndani ya jamii.
Akitumia
zaidi ya dakika 30 akiwa amepiga magoti kunadi sera za CCM na kuomba wananchi
kukipigia kura za ndio CCM kupitia wagombea wake, Mgombea Ubunge katika Jimbo
la Peramiho, Jenista Mhagama akiwa katika Kata ya Kizuka katika Wilaya ya
Songea Vijijini amesema Mgombea wa nafasi ya Urais Tanzania Dkt. Samia Suluhu
Hassan anayo nia njema ya kuimarisha huduma za kinga kupitia wahudumu hao wa
afya ngazi ya jamii.
“Mgombea
wa urais wetu pamoja na kuongeza ajira za watumishi wa afya, kupitia Serikali
tayari alishaanzisha kundi la wahudumu maalum wanaojulikana kama wahudumu wa
afya ngazi ya jamii, na hapa tayari wameshachukuliwa na kupata mafunzo na kazi yao
kubwa ni kupita nyumba kwa nyumba kutoa huduma za afya kwa haraka,” amesema
Mhagama.
Amesema
kuwa wahudumu wanamchango mkubwa katika kuimarisha huduma za kinga ndani ya
jamii ambapo pia husaidia katika kutambua na kushiriki katika jitihada za
udhibiti dhidi ya magonjwa ya mlipuko hatarishi yanayoweza kuleta athari kwa
wananchi.
“Wahudumu
hawa ni watoto wetu, wataendelea kuhudumiwa na Serikali ya CCM, watalipwa posho
na Serikali, na huyu ndiyo jabali mbobezi Dkt. Samia Suluhu Hassan,” amesema
Mhagama.
Mhagama
amewaomba wananchi ifikapo Otoba 29, 2025 kwenda kukipigia kura za ndio CCM
kupitia wagombea wake kuanzia mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, yeye mwenyewe anayeombea nafasi ya Ubunge pamoja
na Madiwani wanaogombea kupitia CCM ili waendelee kuwaletea maendeleo wananchi.
Kupitia
Programu hii iliyozinduliwa mwaka 2024, kiasi cha zaidi ya Shilingi Bilioni 899
kimepangwa kutumika ndani ya miaka mitano kwa ajili ya mafunzo ya darasani na
vitendo, ununuzi wa vitendea kazi pamoja na kulipa posho za wahudumu zaidi ya
137,294 ambao wataajiliwa katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara.



0 Maoni