Wakulima kuweni mabalozi wa mafunzo ya kukuza ujuzi - Zuhura

 

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Zuhura Yunus, amewataka wakulima wadogo na wasindikaji wa zao la zabibu kuwa mabalozi wa mabadiliko chanya ili kukuza ujuzi wa kuongeza thamani ya mazao kwenye mnyororo wa mazao ya kilimo.

Zuhura Yunus ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya kuongeza ujuzi kwa wakulima na wasindikaji wadogo katika sekta ya kilimo leo (21 Oktoba, 2025) jijini Dodoma, yanayolenga kuongeza weledi na ujuzi kwa wakulima wapatao 1,000 nchini.

“Lengo kuu la mafunzo haya ni kuongeza ufanisi katika uzalishaji, kuimarisha njia za utendaji kazi ili kuongeza ubora wa bidhaa na kutoa huduma bora zaidi katika sekta ya kilimo,” alisema Naibu Katibu Mkuu Zuhura Yunus.

Aidha, amesema wakulima na wazalishaji wadogo huchangia katika uzalishaji wa mazao ya chakula nchini na kutoa malighafi kwa viwanda, lakini wamekuwa na changamoto ya upungufu wa ujuzi wa mnyororo wa thamani, ndiyo maana Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu imeandaa mafunzo hayo kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo.

Wakizungumza kwa niaba ya washiriki, Bi. Mary Uguzi ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwapatia ujuzi wenye tija. Naye Noha Madeje amesema kuwa kupitia mafunzo waliyopata wamejifunza vitu vingi katika utengenezaji bora wa mvinyo. Hata hivyo, wanufaika hao wameiomba Serikali kuendelea kuwapatia mikopo itakayowawezesha kukuza biashara zao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Dkt. Thomas Bwana, ambaye anaongoza timu ya wataalam kufundisha wakulima hao, aliwashauri kuwa watumie elimu na ujuzi watakaoupata kwenda kuwafundisha wenzao ili tija inayokusudiwa iweze kupatikana.

Dkt. Bwana aliongeza kusema kuwa TARI imejipanga kuhakikisha matokeo ya tafiti wanazozifanya yanawafikia na kuwasaidia wakulima na wasindikaji wa bidhaa za kilimo nchini ili tija ipatikane na kuchangia ukuaji wa uchumi.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ajira na Ukuzaji Ujuzi, Alana Nchimbi, alieleza kuwa mafunzo haya baada ya kufunguliwa leo, yatatolewa katika mikoa minne na aina ya mazao yatakayohusika kwenye mafunzo hayo ni: Dodoma – Zabibu,Singida – Alizeti, Iringa – Nyanya na mchicha lishe na Mbeya – Maharage na parachichi, ambapo jumla ya wakulima 250 kwenye kila mkoa watanufaika.

Alana aliongeza kuwa Ofisi hiyo inaratibu mafunzo hayo kwa kushirikiana na wadau ili kuwezesha nguvu kazi katika sekta mbalimbali kupata ujuzi stahiki kupitia Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi (Up-skilling Training) kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Chapisha Maoni

0 Maoni