Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA),
imekabidhiwa gari aina ya Toyota Land Cruiser Pick -up na Kampuni ya Magellan
General Trading LLC, kwa ajili ya kuimarisha doria za ulinzi wa rasilimali ya
wanyamapori katika Hifadhi ya Mkungunero.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya gari hilo
yaliyofanyika Oktoba 9,2025, katika Hifadhi ya Mkungunero, Mwakilishi wa
Kampuni ya Megallan General Trading LLC, Ahmed Wasama alisema, wao kama
wawekezaji mahiri katika Hifadhi ya Mkungunero wametoa gari hilo ili kuendelea
kuimarisha shughuli za uhifadhi katika hifadhi hiyo.
Aidha, aliongeza kuwa Megallan itaendelea
kushirikiana na TAWA katika masuala yote ya ulinzi, uboreshaji wa miundombinu
ya utalii iliyopo katika Hifadhi sambamba na kuendelea kutoa elimu ya uhifadhi
kwa vijiji vinavyoizunguka Hifadhi ya Mkungunero.
Kwa upande wake, Kamanda wa Hifadhi ya Mkungunero
Floravick Kallambo ambaye alimwakilisha Kaimu Kamishna wa Uhifadhi - TAWA,
aliishukuru uongozi wa Kampuni ya Megallan General Trading LLC, kwa kuwapatia
gari hilo. Aidha, aliongeza kuwa gari hili litaboresha ufanisi katika shughuli
za doria sambamba na kusaidia katika muitikio wa haraka wa matukio mbalimbali
ya migongano baina ya wanyamapori na wananchi wanaopakana na hifadhi.
Hifadhi ya Mkungunero inapatikana katika Wilaya ya
Kondoa, Mkoa wa Dodoma na imesheheni vivutio mbalimbali ikiwemo mandhari ya
kuvutia na wanyamapori mbalimbali kama vile Tembo, Nyati, Twiga, Pofu, Kudu,
Choroa na Pundamilia.



0 Maoni