Chunya waiomba serikali kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea

 

Katika ziara ya Uhamasishaji wa Matumizi sahihi ya Mbolea Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, inayoongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Dkt. Steven Nindi, uongozi wa Wilaya ya Chunya umeomba wataalam wa Kilimo kuongeza wigo wa kutoa elimu ya Matumizi sahihi ya Mbolea kwani Kilimo ni sayansi na matumizi ya Mbolea yanahitaji vipimo sahihi kulingana na afya ya udongo.

Rai hiyo imetolewa leo tarehe 04.10.2025 katika kikao kilichofanyika katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mkoani Mbeya ambapo Mkuu wa Wilaya ya Chunya SACI Mbaraka Batenga ameeleza kuwa upimaji wa afya ya udongo ni muhimu unamwezesha mkulima kuwa na utaalam, kutumia mbolea kwa usahihi na kuongeza uzalishaji wa mazao.

“Msimu wa Kilimo ulioisha mwaka 2024/2025, zao la tumbaku limefanya vizuri, mbolea iliyosambazwa na TFC imeongeza uzalishaji zaidi ya makadirio yaliyokuwepo ambapo Wilaya ya Chunya imezalisha tani milion 27,091.7 na kuondoa malalamiko kwa wakulima,” ameeleza SACI Batenga.

Pamoja na mafanikio hayo ameeleza kuwa bado yapo maeneo ambayo hayana mwamko wa kutumia mbolea kama eneo la kata ya Kambi Katoto na Sipa hivyo endapo watapewa elimu ya matumizi ya Mbolea watahamasika kutumia mbolea na kuongeza uzalishaji.

Kwa upande wake Dkt. Stephen Nindi amepongeza juhudi za viongozi kuhakikisha wanapata mashine za kupimia afya ya udongo ili kumrahisishia mkulima kutambua aina ya udongo na mbolea inayopaswa kutumika.

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) Ndg. Samuel Mshote ameeleza kuwa katika msimu wa Kilimo uliopita TFC ilisambaza tani 61,000 ya Mbolea ya NPK 10:18:24 kwa wakulima wa zao la tumbaku na kwa mwaka huu wa TFC itasambaza takribani tani 71,000 za mbolea ya NPK 10:18:24 inaendelea kusambazwa kwa wakulima kupitia vyama vyao vya ushirika.

Aidha, Ndg. Mshote ameeleza kuwa hadi sasa usambazaji wa mbolea ya NPK 10:1824 kwa Wilaya ya Chunya umefikia asilimia 85, tani 10,395 zimewafikia wakulima kati ya tani 12,230 zinazotarajiwa kusambazwa katika msimu huu. Na kwa mbolea ya UREA na CAN tayari zipo Nchini na zitaanza kusambazwa kWa wakulima ndani ya mwezi huu wa Oktoba, 2025.




Chapisha Maoni

0 Maoni