Septemba 2024, jina la Bilionea Aidan Andrea Msigwa
lilitikisa Sekta ya Madini kama radi katikati ya jua kali kwa kuuza kilo 111.82
za dhahabu. Alivuna zaidi ya shilingi bilioni 20.11 kwa mkupuo mmoja hatua
iliyotikisa si tu wadau wa madini, bali iliwaamsha Watanzania wengi hadi kuvuka
mipaka ya nchi. Aidan hakutajwa tu kama gwiji wa madini, bali aliwekwa rasmi
kwenye meza ya mabadiliko ya kiuchumi ndani na nje ya Tanzania.
Baada ya kuvuna mabilioni kutokana na kuuza dhahabu
hiyo Aidan hakukimbilia anasa bali alichagua kuwekeza kwa watu baada ya kutumia
kiasi kikubwa cha fedha kuinunua Kampuni ya SUNSHINE Group iliyoko Matundasi
Chunya iliyokuwa ikimilikiwa na wawekezaji kutoka China. Kwa sasa yupo mbioni
kwa kushirikiana na wawekezaji wengine wa China kukifufua kiwanda hicho kikubwa
cha kuchenjua dhahabu kilichokuwa kimesimamisha shughuli zake kwa takribani
miaka miwili. Kiwanda hicho kinatarajiwa kuchukua miezi miwili ya ukarabati
baada ya taratibu za kiuwekezaji kukamilika. Aidha, kinatarajia kuchenjua tani
500 kwa saa 24, kuzalisha zaidi ya ajira 350 kwa watanzania huku kwa wageni
zimetengwa nafasi 40 tu ambapo chini ya ubia huo, wanatarajia kuleta
teknolojia.
Anasema mbali ya kuinunua SUNSHINE fedha nyingine
aliwekeza kwenye ununuzi wa vifaa kwa ajili ya kuendeleza shughuli zake za
uchimbaji na uchakataji madini kama ununuzi wa escavetor, magari na mitambo
mingine ya kurahisisha kazi zake. Pia, Aidan ni mmiliki wa leseni kadhaa za
uchimbaji mdogo wa madini na anazo leseni nyingine ambazo zina uzalishaji lakini bado hajaanza kuchimba na anaweza
kushirikiana na mwekezaji. Vilevile,
anao mtambo wa kuchakata dhahabu
wenye uwezo wa kuchakata tani Mia Mbili 200 kwa saa 24.
Hadithi ya Aidan si ya mtu mmoja kutengeneza
mabilioni, bali ni simulizi ya kizalendo ya mtu kurejesha matumaini kwa mamia
ya familia, vijana, na jamii zinazotegemea Sekta ya Madini kama chanzo cha
maisha. Katika mahojiano maalum na timu ya Madini Diary, amefunguka
juu ya safari yake, maono yake, na kwa nini anasema huu ni mwamko mpya
wa kiuchumi na unaong’aa kama jua la asubuhi kwa Chunya na Tanzania.
Aidan anasema hakuwahi kufika sekondari. Elimu yake
rasmi iliishia darasa la saba, lakini ndoto zake hazikuishia darasani. Tangu
mwaka 1989, alihangaika kwenye machimbo, makarasha, kuchenjua, akijifunza kwa
vitendo, akikosea na kujirekebisha, akipigania maisha kwa jasho la kweli la
mchimbaji mdogo.
Lakini leo, licha ya kuvuna bilioni 20.11 za mkupuo
na kipato kingine kutoka vyanzo vingine vya uchimbaji, anasema jambo moja
analojutia ni kutokuendelea na shule. “Sasa hivi nikikutana na wageni kama hawa
mnaowaona, nasemewa na wengine… hilo huwa linaniumiza sana kwasababu ningeweza
kuzungumza mwenyewe. Hiki ni kitu ninachojutia kweli japo nilitamani kufanikiwa
kwa haraka,” anasema kwa utani wenye uzito. Ndiyo maana licha ya mafanikio
yake, anasisitiza kwa nguvu: “Usiache shule kwa tamaa ya mafanikio ya haraka.
Mafanikio yatakuja, lakini elimu ni msingi wa kudumu,’’ anasema Aidan.
Licha ya kuvuna bilioni 20.11 kwa mkupuo mmoja,
Aidan Msigwa hakubadilika. Anasema wazi, “Mimi tarehe zote huzimalizia porini
si mtu wa starehe, kuanzia tarehe 1 hadi 30, niko porini.”
Badala ya kupumzika, aliona mafanikio hayo kama
hatua ya kwanza ya kuongeza bidii zaidi. Yalimwinua yakamweka mbele ya jamii
kama mfano wa kweli, mtu wa kawaida aliyefanikisha ndoto kubwa kwa uvumilivu,
uaminifu, na juhudi za kweli. Wengi sasa wanamchukulia kama kioo, wakiona ndani
yake picha ya matumaini yao. Amewapa nguvu ya kupambana zaidi, na kwa kiasi
kikubwa, amechochea wimbi jipya la uchimbaji na uwekezaji Chunya si kwa
wachimbaji wadogo pekee, bali hata wawekezaji wa ndani na nje wanaotaka kuwa
sehemu ya hadithi yake. Kwa Aidan alama aliyoiweka haitoshi anataka kwenda
mbele zaidi na anasema wachimbaji wadogo wataleta mabadiliko Tanzania.
Ombi kwa tasisi za fedha na Serikali
Kutokana na mazingira ya shughuli za madini Aidan
anatoa ombi kwa taasisi za fedha kuwaamini wachimbaji na wasipewe masharti sawa
na wawekezaji wengine kutokana na uhalisia wa shughuli za madini. Pia, anatoa ombi
kwa Serikali kutokuhesabu madeni ya nyuma
baada ya kuanzishwa utaratibu mpya wa kutozwa asilimia 2 za Mamlaka ya
mapato Tanzania (TRA) katika yote Msigwa hakuacha kuishukuru Serikali kwa
kuwezesha mazingira yaliyomfikisha alipo.
Na hii kwa ufupi ndiyo SIMULIZI ya Aidan Andrea
Msigwa mmiliki wa Kampuni ya Mdimi
Investment, kutoka darasa la Saba hadi Bilioni 20.11: Safari ya uaminifu,
uvumilivu na sasa SUNSHINE. Simulizi zaidi
ya Aidan ifuatilie hivi karibuni kupitia Madini Diary.
Vision 2030: Madini ni Maisha na Utajiri


0 Maoni