Wananchi 814 wahudumiwa banda la TARURA, Maonesho ya Madini - Geita

 

Wananchi wapatao 814 wamehudumiwa kwenye banda la Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) katika Maonesho ya Nane ya Kitaifa ya Madini yaliyomalizika mwishoni mwa wiki mkoani Geita.

Afisa Ustawi wa Jamii kutoka TARURA mkoa wa Geita, Bw. Godfrey Vedasto amesema wananchi hao walifika katika banda la Wakala huo kupata elimu kwa ujumla ya namna wanavyotekeleza majukumu yao lakini pia kupata uelewa wa namna wanavyoshughulikia utatuzi wa ubovu wa barabara katika maeneo yao.

“Jumla ya wananchi 814 walitembelea banda letu, wanaume 444 na wanawake 374, wengi walitupongeza kwa kazi kubwa tunayoifanya ya kufungua barabara katika maeneo yao, pia wengine walitaka kufahamu namna tunavyoweza kutatua changamoto za ubovu wa barabara katika maeneo yao.”

Amesema pia wananchi walitaka kupata uelewa kuhusu fidia katika miradi inayokusudiwa kutekelezwa na Wakala huo.

“Ipo miradi ambayo wananchi hulipwa fidia, sisi kama TARURA huwa tunatoa elimu kabla ya mradi kutekelezwa, sema wapo baadhi ya wananchi bado wanahitaji elimu zaidi”, ameongeza kusema.

Hata hivyo, amesema elimu ya utunzaji wa miundombinu ya barabara ilitolewa na kuwakumbusha wananchi waendelee kuwa mabalozi wazuri wa kulinda barabara pamoja na mitaro ya maji ili idumu muda kwa mrefu.

Amemaliza kwa kusema kwamba maonesho hayo kwa TARURA yamekuwa na tija kubwa kwani wameweza kuwafikia wananchi wengi na kutatua changamoto zao katika maeneo yao.



Chapisha Maoni

0 Maoni