Imeelezwa
kwamba Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) hufanya usanifu wa
kina wa barabara kabla ya ujenzi kuanza kutekelezwa.
Hayo
yamebainishwa na Mhandisi wa miradi kutoka TARURA Faizer Mbange wakati akitoa
elimu kwa umma kwa wananchi waliofika kwenye Maonesho ya Nane ya Madini Mkoani
Geita.
Amesema
kwamba barabara nyingi nchini
zinazosimamiwa na Wakala kwa sasa zina hali nzuri kwani usanifu wa kina
hufanyika pamoja na usimamizi madhubuti wakati wa utekelezaji wa mradi.
“Yote
haya yanafanyika ili kuhakikisha thamani
na viwango vya barabara vinafikiwa ili kukidhi mahitaji na kupata
thamani ya fedha iliyokusudiwa katika ujenzi wa miundombinu”.
Naye,
Afisa Ustawi wa Jamii Mwandamizi kutoka TARURA Mkoa wa Geita Bw. Godfrey
Vedasto amewataka wananchi kuendelea kutunza miundombinu ya barabara
zinazotengenezwa katika maeneo yao ili
zidumu kwa muda mrefu.
Amesema
serikali inatumia fedha nyingi katika ujenzi wa miundombinu ya barabara ikiwemo
mitaro ya maji hivyo wananchi wanapaswa kuitunza na kutofanya shughuli kwenye
maeneo ya hifadhi ya barabara.
“Shughuli
kwenye hifadhi ya barabara zikiwemo kutupa taka kwenye mitaro ya maji na hivyo
msimu wa mvua mitaro hiyo hujaa uchafu na kusababisha mafuriko”.
Amesema
mafuriko hayo husababisha maji kujaa kwenye makazi ya watu, kuharibu barabara
na kusababisha milipuko ya magonjwa mbalimbali.
Pia Mkazi
wa Geita Bw. Augustino Stephano ameipongeza TARURA kwa ujenzi wa barabara za
mitaa pamoja na mitaro kwani hivi sasa barabara zinapitika kwa urahisi.
Amesema elimu waliyoipata kutoka kwa wataalam wa
TARURA itawasaidia katika utunzaji wa mitaro na barabara na kutoa rai kwa wananchi wengine kutoa
ushirikiano kwa Wakala huo kutunza miundombinu katika maeneo yao.



0 Maoni