Kiwanda
cha kusafisha madini ya dhahabu cha Mwanza Precious Metals Refinery (MPMR)
kilichopo jijini Mwanza, kimefanikiwa kukusanya zaidi ya tani tano za dhahabu
kwa niaba ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT).
Hayo
yamesemwa na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Nyaisara Mgaya,
alipokuwa akizungumza na ujumbe kutoka nchini Malawi uliotembelea mkoani humo
kwa lengo la kujifunza kuhusu usimamizi na uendeshaji wa biashara ya madini,
hususan mfumo wa masoko unaotumika nchini Tanzania.
Mhandisi
Mgaya amesema kuwa kiwanda hicho kina uwezo wa kusafisha hadi kilo 960 za
dhahabu kwa siku, ingawa kwa sasa kinatumia mashine zenye uwezo wa kusafisha
kilo 480 kwa siku, kutokana na upatikanaji wa malighafi.
Katika
kikao hicho, kiongozi wa ujumbe kutoka Malawi, ambaye pia ni Mkurugenzi
Mtendaji wa Maendeleo ya Biashara za Vikundi nchini humo, Zizwan Khonje,
amemshukuru Afisa Madini wa Mkoa wa Mwanza kwa elimu waliyoipata kuhusu mfumo wa
biashara na masoko ya madini hapa nchini.
“Tanzania
ni mfano wa kuigwa katika ukanda wa Afrika Mashariki kutokana na hatua
mbalimbali ilizochukua katika kuboresha Sekta ya Madini, ikiwemo uanzishwaji wa
masoko ya madini ya wazi na matumizi ya mifumo ya kidijitali katika usimamizi
wa rasilimali hizi,” amesema Khonje.
Awali,
ujumbe huo ulipata nafasi ya kutembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, ambako
walipokelewa na Katibu Tawala wa Mkoa huo Bw. Balandya Elikana, ambaye
aliwakaribisha rasmi mkoani humo.
Ziara
hiyo ya ujumbe kutoka Malawi inatarajiwa kuwa chachu ya mabadiliko katika sekta
ya madini ya nchi hiyo kwa kuimarisha mifumo ya uwazi, kuongeza mapato ya
serikali, na kuwezesha ushirikishwaji wa wachimbaji wadogo kwenye soko la
kimataifa la madini.



0 Maoni