TBN yatambulika rasmi MCT, yajipanga kutetea wanablogu

 

Mtandao wa Wanablogu Tanzania (TBN) umepiga hatua kubwa katika safari yake ya kuhalalishwa kitaaluma baada ya kukabidhiwa rasmi hati za uanachama wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), katika Mkutano Mkuu wa 27 wa Baraza hilo uliofanyika Septemba 25, 2025, jijini Dar es Salaam.

TBN ni miongoni mwa wanachama wapya wanane waliojiunga na Baraza hilo, hatua inayotajwa kuwa ya kihistoria katika kuimarisha sauti na nafasi ya wanablogu katika tasnia ya habari nchini.

Akizungumza mara baada ya hafla ya makabidhiano, Mwenyekiti wa TBN, Beda Msimbe, alisema uanachama huo ni zaidi ya heshima ni chombo cha ulinzi na utetezi wa haki za wanablogu.

"Uanachama huu unatoa uhalali na kutambuliwa rasmi kwa wanablogu mbele ya jamii, Serikali na wadau wengine. Tunajumuishwa katika familia kubwa ya vyombo vya habari vinavyojisimamia, na sasa wanablogu wanatambulika kama chanzo cha habari kinachowajibika," alisema Msimbe.

Msimbe alibainisha kuwa kupitia MCT, wanablogu sasa wana fursa ya kunufaika na mfumo wa usuluhishi wa Baraza, hususan katika kushughulikia malalamiko yanayoweza kujitokeza kutokana na kazi zao.

"Mfumo huu unawalinda wanablogu kisheria na kiuchumi dhidi ya vitisho au kufilisiwa kutokana na faini za kimahakama, kwa kuwa sasa wana kimbilio katika Kamati ya Maadili ya MCT," aliongeza.

MCT Yasisitiza Mshikamano wa Wanachama

Katibu Mtendaji wa MCT, Ernest Sungura, alisisitiza kuwa mafanikio ya Baraza yanatokana moja kwa moja na uimara wa wanachama wake.

"Kauli mbiu ya mwaka huu inasema ‘Uhai wa Wanachama ni Nguvu na Usalama wa Taaluma ya Habari’. Ikumbukwe ni wanachama waliokubaliana kwamba tujisimamie au tukubali kufa," alisema Sungura.

Alionya kuwa enzi za kutegemea wafadhili zimeshaisha, na sasa Baraza linategemea wanachama wake kwa uhai na maendeleo yake.

Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya MCT, Yusuf Khamis Yusuf, alisisitiza kuwa kwa miaka 30 tangu kuanzishwa kwa Baraza hilo mwaka 1995, limejipambanua kama nguzo ya maadili na weledi nchini.

"Kusimama na Haki ni Sadaka" – Jaji Mihayo

Mkutano huo ulifunguliwa rasmi na Jaji Mstaafu Thomas Mihayo, Rais Mstaafu wa Nne wa Baraza, ambaye aliwakumbusha wanahabari kuhusu dhamana waliyo nayo mbele ya jamii. 

"Kusimama kwenye haki ni kugumu kuliko kujipendekeza. Kusimama na haki kunahitaji sadaka. Siyo njia nyepesi au rahisi, lakini ni njia ya baraka mno na ni njia inayompendeza Mungu," alisisitiza Jaji Mihayo.

Alieleza kuwa uwepo wa MCT umeokoa vyombo vingi vya habari dhidi ya kufilisiwa, na kwamba ni jukumu la kila chombo wakiwemo wanablogu  kuwa kiungo cha ukweli bila kuegemea upande wowote.

Katika hatua nyingine muhimu, Jaji Mihayo alizindua rasmi Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT 2025), ambazo mwaka huu zitaendeshwa kwa mfumo wa kidijitali sambamba na uzinduzi wa tovuti mpya ya MCT hatua inayoashiria dhamira ya Baraza katika kukuza weledi na teknolojia kwenye tasnia ya habari.



Chapisha Maoni

0 Maoni