Naibu
Kamishna wa Uhifadhi, Huduma za Shirika la Hifadhi ya Ngorongoro, Bw. Aidan
Makalla ameongoza ujumbe wa shirika hilo kushiriki katika maonesho ya “My
Tanzania Roadshow 2025 Europe”, yenye lengo la kunadi fursa za utalii na
uwekezaji katika hifadhi hiyo maarufu duniani.
Bw.
Makalla ameambatana na Afisa Utalii Mkuu Msaidizi, Bw. Abdiel Laizer, ambapo
wameshiriki kwenye mikutano na majadiliano na mawakala mbalimbali wa utalii
kutoka barani Ulaya katika miji ya Stuttgart (Ujerumani), Salzburg (Austria),
Ljubljana (Slovenia) na Milan (Italia) kuanzia Septemba 22 hadi 27, 2025.
Maonesho
hayo yaliyoandaliwa na Kampuni ya KILIFAIR, yanatajwa kuwa miongoni mwa
majukwaa ya kipekee ya kutangaza vivutio vya utalii wa Tanzania, yakilenga
kuitangaza nchi kama kitovu cha utalii barani Ulaya.
Takriban
kampuni 80 kutoka Tanzania na Ujerumani zinashiriki katika maonesho hayo,
zikiwemo kampuni binafsi, taasisi za kiserikali na mashirika ya kimataifa ya
utalii.
Maonesho
ya "My Tanzania Roadshow" yanatarajiwa kusaidia kwa kiasi kikubwa
kuongeza mwamko wa watalii kutoka bara la Ulaya kuitembelea Tanzania, hususan
Hifadhi ya Ngorongoro, Serengeti, Ziwa Natron na maeneo mengine yenye vivutio
vya kipekee.



0 Maoni