Tukishinda NRA, tutatoa bure mashine za EFD kwa wafanyabiashara

 

Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha National Reconstruction Alliance (NRA), Almas Kisabya, ameahidi kutoa mashine za kielektroniki za ukusanyaji mapato (EFD) bure kwa wafanyabiashara wote nchini, ikiwa atachaguliwa kuongoza serikali.

Kisabya alitoa kauli hiyo jana, Jumapili Septemba 7, 2025, wakati wa uzinduzi rasmi wa kampeni za chama hicho uliofanyika katika eneo la Soko la Matunda, Kata ya Chem Chem, Manispaa ya Tabora.

“Ndani ya siku 30 tu baada ya kuunda Baraza la Mawaziri, kipaumbele chetu kitakuwa kuhakikisha EFD zinatolewa bure kwa wafanyabiashara kote nchini. Hili ni jukumu la serikali, si mzigo wa mwananchi,” alisema Kisabya.

Aidha, mgombea huyo alieleza kuwa chama chake kinapanga kuhusisha mashirika ya umma kama Tanesco katika mfumo wa ukusanyaji wa mapato, akisema taasisi hiyo imeonesha mafanikio makubwa katika udhibiti wa makusanyo bila kuathiri mahusiano yake na wateja.

“Ikiwezekana, Tanesco tutawatumia kusaidia katika ukusanyaji wa mapato, maana wameweza kufanikisha makusanyo yao bila migogoro na wananchi,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine, Kisabya aliahidi kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji bure, kwa kutumia mitambo ya nishati jadidifu kama sola na upepo katika kusambaza maji vijijini na mijini.

“Utaalamu upo, teknolojia ipo. Tukitumia mfumo huu, gharama za upatikanaji wa maji zitashuka kwa kiasi kikubwa. Tunataka kuhakikisha kila Mtanzania anapata maji safi bila kikwazo,” alisema.

Kampeni za NRA zimezinduliwa kwa kaulimbiu ya "Tanzania Mpya, Maisha Bora Kwa Wote", huku mgombea huyo akiahidi kuwa chama chake kitatoa kipaumbele kwa miradi ya kijamii inayogusa maisha ya wananchi wa kawaida.

Chapisha Maoni

0 Maoni