Mgombea urais NLD awataka wakazi wa Muheza kutoipa kura CCM

 

Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha National Liberal Democratic (NLD), Doyo Hassan Doyo, ameendelea na kampeni zake za kijiji kwa kijiji na kata kwa kata, akiwataka Watanzania kufanya mabadiliko ya kweli kupitia sanduku la kura.

Akihutubia wakazi wa Kata ya Majengo, wilayani Muheza, mkoani Tanga, Doyo aliishutumu serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa, kile alichodai, kuwaacha nyuma wananchi wa eneo hilo licha ya mchango wao mkubwa kiuchumi katika mkoa mzima.

“Haiwezekani maji yanayotumika Tanga Mjini yatoke Muheza, lakini wananchi wa Muheza wenyewe wanakosa maji. Hili ni tatizo la muda mrefu linalochangiwa na uongozi wa CCM, ambao kwa miaka mingi umeshindwa kutatua changamoto zenu,” alisema Doyo.

Doyo alieleza kuwa licha ya kuwa Barabara ya Amani ni kiungo muhimu cha uchumi wa eneo hilo, bado imeendelea kusahaulika na kutelekezwa kwa ahadi zisizotekelezwa.

“Viungo kutoka Muheza vinauzwa hadi nje ya nchi kwa fedha za kigeni, lakini barabara inayosafirisha bidhaa hizo ni mbovu kupita kiasi. Mkichagua NLD, tutahakikisha inakarabatiwa mara moja,” aliahidi.

Kwa upande wake, Mkomwa, mmoja wa viongozi wa chama hicho, alisema wananchi wa Muheza wana sababu nyingi za kuunga mkono NLD, akitaja miundombinu duni, ukosefu wa ajira kwa vijana, na ugumu wa maisha kwa akina mama kuwa miongoni mwa changamoto zinazopaswa kushughulikiwa kwa haraka.

Naye Mkurugenzi wa Habari na Mahusiano ya Umma wa NLD, Pogora Ibrahim Pogora, alitoa wito kwa wakazi wa Muheza kujitokeza kwa wingi kupiga kura katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, na kutumia fursa hiyo kuiondoa CCM madarakani.

“Hakuna namna CCM inaweza kujitenga na hali duni ya maisha ya Watanzania. Ni chama kilichoongoza kwa muda mrefu lakini bado wananchi wanateseka. Sasa ni muda wa mabadiliko,” alisema Pogora.

Kampeni za Chama cha NLD zilianza rasmi Septemba 4 mkoani Tanga, na zinaendelea katika maeneo mbalimbali ya nchi. Baada ya ziara ya Muheza, msafara wa mgombea huyo wa urais unatarajiwa kuelekea Korogwe, Lushoto na Handeni.

Chapisha Maoni

0 Maoni