Mwiru: Sitapenda kuona Mtanzania anaishi kwenye nyumba ya nyasi

 

Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Wakulima (AAFP), Kunje Ngombale Mwiru, amesema kuwa endapo atapata ridhaa ya kuongoza nchi katika Uchaguzi Mkuu wa 2025, hatapenda kuona Mtanzania yeyote anaendelea kuishi kwenye nyumba ya nyasi.

Mwiru alitoa kauli hiyo Septemba 2, 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika kata ya Matombo, Jimbo la Morogoro Kusini, akitokea kata ya Kisaki, ambako alikuwa akihutubia wananchi na kuelezea vipaumbele vyake iwapo atachaguliwa kuwa Rais.

“Ndugu zangu, maendeleo hayahitaji hasira wala jazba. Kwa kipindi changu cha miaka mitano, sitapenda kuona Mtanzania yeyote anaishi kwenye nyumba za nyasi, iwe ni mwana-Matombo au wa sehemu nyingine yoyote nchini,” alisema Mwiru.

Alisema kuwa Tanzania ina viwanda vya kutosha vya kuzalisha mabati, hivyo kupitia ushirikiano na viongozi wa wilaya na mikoa, ataweka utaratibu wa kubaini idadi ya wananchi wanaoishi kwenye nyumba za nyasi ili kuhakikisha wanajengewa nyumba zenye mabati.

Miundombinu, mawasiliano na ajira kwa vijana

Mbali na makazi bora, Mwiru alisema serikali yake itahakikisha kila kaya inapata huduma ya mawasiliano ya simu ili kuwawezesha wananchi kuwasiliana moja kwa moja na viongozi wao wa ngazi ya wilaya na mkoa.

“Serikali yangu itakuwa ya mchakamchaka, ya saa 24. Itafanya kazi bila kupumzika. Hii itaongeza ajira kwa vijana. Sio kwamba ajira hakuna, bali mazingira ya vijana kupata ajira ndio hayajatengenezwa,” alisisitiza.

Mwiru alieleza kuwa ana mpango wa kuanzisha viwanda vya kuchakata vyakula, matunda na hata kuchonga mawe maeneo ya vijijini ili kutoa ajira kwa vijana bila kulazimika kwenda Dar es Salaam.

“Ile dhana ya kwamba mtu lazima aende Dar es Salaam kutafuta kazi viwandani si ya kweli. Hata huku kwetu kuna sifa za kuanzisha viwanda. Tutatengeneza mazingira bora ya uwekezaji vijijini,” aliongeza.

Walimu na wastaafu kupewa kipaumbele

Katika hotuba yake, Mwiru aliweka msisitizo maalum kwa walimu, akisema kuwa serikali yake itawajengea nyumba bora, kuboresha mazingira yao ya kazi na kuongeza mishahara yao kwa kutambua mchango wao katika jamii.

“Mwalimu ndiye anayemfundisha Profesa, hata fisadi. Kwa hiyo, mwalimu anapaswa kupewa heshima kubwa, si kuishi kwenye nyumba za buibui bila umeme. Serikali yangu haitavumilia hali hiyo,” alisema.

Aidha, alisema wastaafu wenye afya njema wataendelea kushiriki katika kazi za kuimarisha taifa kupitia mafundisho ya uzalendo na maadili, huku akiweka mpango wa kuanzisha madarasa maalum ya kuwahusisha katika kutoa elimu hiyo kwa vizazi vijavyo.

“Tutawawezesha wastaafu wanaoweza kufanya kazi waendelee kufundisha uzalendo na maadili. Huu ndio msingi wa Taifa imara,” alisema.

Awataka wakulima kutokubali kudanganywa

Akihitimisha hotuba yake, Mwiru aliwataka wakulima kujitambua na kutokubali kudanganywa na wanasiasa wa vyama vingine, akisisitiza kuwa AAFP ni chama chao halisi.

“Msidanganywe kwamba kuna mwanasiasa wa chama kingine atakayekuja kuwasemea wakulima. Kama mkitutosa AAFP, mmewatosa wakulima wenzenu. Chagueni chama chenu, mchagueni mkulima mwenzenu,” alihitimisha.



Chapisha Maoni

0 Maoni