Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa kushirikiana na wadau wengine wa Uhifadhi mkoani Kagera limeanza rasmi operesheni ya kuwahamisha Tembo zaidi ya 500 waliokuwa kwenye Bonde la Kitengule, na kuwapeleka Hifadhi ya Taifa Burigi–Chato. Hatua hiyo inalenga kulinda maisha ya wananchi, mali zao, pamoja na mashamba ya wakulima na wawekezaji kutokana na uharibifu uliokuwa ukisababishwa na wanyama hao.
Zoezi hilo
limezinduliwa jana tarehe 2 Septemba 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Hajat
Fatma Mwassa, katika viwanja vya Kiwanda cha Sukari Kagera. Amewahakikishia
wananchi kwamba changamoto na madhara yaliyokuwa yakisababishwa na Tembo
kuvamia makazi na mashamba sasa yanakwenda kufika kikomo.
"Mhe.
Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amefanya kazi
kubwa ya kuhakikisha wanyama hawa aina ya Tembo wanahamishwa kurudishwa kwenye
Hifadhi ya Taifa Burigi-Chato, aidha ametuma wataalam na helikopta ili
kuwahamisha Tembo zaidi 500 waliopo katika Bonde la Kitengule,"
alisisitiza Mkuu wa Mkoa Mhe. Mwassa.
Kwa upande
wake, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Dkt. Fredrick Mofulu, amewahakikishia
wananchi usalama katika zoezi zima la kuwahamisha Tembo hao.
0 Maoni