Ujenzi wa
Barabara ya Buhongwa-Igoma yenye urefu wa Km 14 kwa kiwango cha lami
inayojengwa katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza inatajwa kuwa ndio mwarobaini
wa changamoto ya msongamano wa magari jijini humo.
Hayo
yamesemwa na Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza Wakili Kiomoni Kibamba wakati
akielezea hali ya utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa katika Jiji
la Mwanza kupitia Mradi wa Uendelezaji Miji na Majiji Tanzania (TACTIC) na manufaa yake kwa wananchi.
Amesema
barabara hiyo inayounganisha Kata nne ambazo ni Buhongwa, Lwanhima, Kishiri na
Igoma ilikuwa na changamoto kubwa hali iliyopelekea magari yote yaliyokuwa
yakitoka Buhongwa kwenda Igoma au Igoma kwenda Buhongwa kulazimika kuingia
katikati ya jiji hivyo kuongeza msongamano wa magari.
Wakili
Kibamba ameongeza kuwa ujenzi wa
barabara hiyo utasaidia kupunguza msongamano huo kwa kiasi kikubwa kwani magari
yote yaliyokuwa yanatoka maeneo hayo hayatolazimika kuingia katikati ya Jiji
badala yake yatakwenda moja kwa moja ama Igoma au Buhongwa.
Vilevile,
Mradi wa (TACTIC) katika Jiji la Mwanza unatekeleza Mradi wa ujenzi wa Soko la
samaki wabichi Kata ya Mkuyuni ambapo kwa mujibu wa Wakili Kibamba amesema kuwa
hiyo ilikuwa ni changamoto iliyokuwa inawakabili kwa muda mrefu.
"Halmashauri
ya Jiji la Mwanza tulikuwa na changamoto ya kukosekana kwa eneo la kuuzia mazao
ya uvuvi. Ujenzi wa soko la samaki la Mkuyuni litawezesha kunyanyua uchumi kwa
sababu hata haya maboti ya uvuvi yanayotoka Wilaya ya Ukerewe na upande wa
Buchosa Wilayani Sengerema yatakuwa yanakuja kuuzia samaki kwenye soko hili,
kwa hiyo tutafungua uchumi sio wa hapa tu lakini pia imesaidia mazingira ya
uwezeshaji wa kufanya biashara kati ya Mwanza na Mikoa mingine,"
amebainisha Wakili Kibamba.
Kwa mujibu
wa Wakili Kibamba miradi yote miwili kwa pamoja sio tu imesaidia kulifanya jiji
la Mwanza kupendeza lakini imepandisha
thamani ya ardhi kwa wananchi sambamba na kurahisisha shughuli za usafirishaji
wa watu na bidhaa kwenye maeneo ya miradi.
Kwa upande
wake Bw. Kalumanzila Idd, Mkazi wa Buhongwa, jijini Mwanza ameishukuru serikali
kwa kuwajengea barabara hiyo kwani imewaondolea adha ya usafiri iliyokuwa
inawakabili kwa muda mrefu.
Naye, Bi.
Judith S. Maningo Mkazi wa Mtaa wa Ihushi, Kata ya Kishiri amesema kuwa pamoja
na Rais Samia kuwapelekea Miradi mingi ya maendeleo lakini ujenzi wa barabara
ya Buhongwa-Igoma umeleta ukombozi mkubwa kwa wana Ihushi na Kishiri kwa
ujumla" amesema.
0 Maoni