Tanzania
imepata heshima kubwa ya kimataifa baada ya kutunukiwa Medali ya Dhahabu katika
Kongresi ya 49 ya Apimondia iliyofanyika katika ukanda wa Scandinavia (Sweden,
Denmark na Norway).
Tuzo hiyo
ilitangazwa Septemba 27, 2025 ambapo banda la Tanzania lilishinda katika
kipengele cha Large Stand (zaidi ya mita 36 za mraba) kutokana na ubunifu na
ubora wa maonesho ya mazao ya nyuki yaliyovutia wageni kutoka mataifa
mbalimbali duniani.
Cheti cha
ushindi kimetolewa na Rais wa Shirikisho la Apimondia, Jeff Pettis, kwa
kutambua mchango wa Tanzania katika kukuza tasnia ya nyuki kimataifa.
Akizungumza
mara baada ya kupokea cheti hicho, Kamishna Msaidizi anayesimamia Rasilimali za
Nyuki, Hussein Msuya, alisema ushindi huo ni ishara kuwa Tanzania imeanza
kuthibitisha nafasi yake kama kitovu cha uzalishaji na usindikaji wa mazao ya
nyuki barani Afrika na duniani.
“Ushindi
huu unatarajiwa kuongeza thamani ya bidhaa za nyuki za Tanzania sokoni, hususan
asali, nta na chavua, na hivyo kuwaongezea kipato wakulima na wajasiriamali
wadogo,” alisema Msuya.
Washiriki
kutoka Tanzania walisema medali hiyo ni matokeo ya juhudi za pamoja kati ya
Serikali, wadau wa sekta binafsi na wafugaji nyuki walioweka mbele ubora,
uendelevu na matumizi bora ya rasilimali za misitu na nyuki nchini.


0 Maoni