Shirikisho
la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA) limepokea mwaliko
rasmi kutoka kwa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Malawi kushiriki
katika Maonesho ya Kwanza ya Teknolojia ya Madini nchini humo, yanayotarajiwa
kufanyika Novemba 2025.
Mwaliko
huo umetolewa na Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Malawi,
Bw. Percy Maleta, wakati wa kikao maalum kilichofanyika katika ukumbi wa
mikutano wa Lenny Hotel mkoani Geita, sambamba na Maonesho ya Nane ya
Teknolojia ya Madini yanayoendelea kaika viwanja vya Samia Suluhu Hassan
Bombambili mkoani Geita.
Akizungumza
katika kikao hicho, Bw. Maleta amesema kuwa Malawi ina utajiri mkubwa wa
rasilimali za madini, lakini bado kuna changamoto ya teknolojia duni, ukosefu
wa mitaji, elimu ya madini na utafiti. Amesisitiza kuwa ushirikiano na FEMATA
unaweza kusaidia kuimarisha sekta hiyo kwa pande zote mbili kwa kubadilishana
uzoefu na maarifa.
"Malawi
ina fursa nyingi kwenye Sekta ya Madini, lakini bado tunahitaji kujifunza
kutoka kwa wenzetu wa Tanzania, hasa katika matumizi ya teknolojia na mifumo
bora ya usimamizi," amsema Maleta.
Katika
ziara yao, ujumbe kutoka Malawi umetembelea Maonesho ya Nane ya Teknolojia ya
Madini 2025 mkoani Geita na kujionea namna Tanzania inavyotekeleza shughuli za
sekta hiyo, hususan katika kuhamasisha matumizi ya teknolojia na ushiriki wa
wachimbaji wadogo.
Akizungumza
kwa niaba ya Rais wa FEMATA, Katibu wa Wachimbaji Madini wa Mkoa wa Shinyanga
(SHILEMA) Gregory Kibusi ameeleza kuwa FEMATA ipo tayari kushirikiana na
Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Malawi katika maeneo mbalimbali ya
maendeleo ya Sekta ya Madini, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kikanda na
kuchochea maendeleo endelevu ya uchumi wa nchi zote mbili.
Katika
hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martin Shigella, amekutana na
ujumbe huo wa Malawi na kushiriki nao katika chakula cha pamoja. Mhe. Shigella
ameukaribisha ujumbe huo mkoani humo na kupongeza juhudi za kujifunza kutoka
kwa Tanzania katika usimamizi wa mifumo ya Sekta ya Madini.




0 Maoni