Naibu
Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo, amesema Serikali kupitia Wizara
inajivunia hatua kubwa iliyopigwa kwa kuongezeka ushiriki wa wanawake kwenye
mnyororo mzima wa madini, hatua inayodhihirisha dhamira ya Serikali ya
kuendeleza usawa wa kijinsia katika sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa taifa.
Ameyasema
hayo leo Septemba 28, 2025, katika Maonesho ya Teknolojia ya Madini Geita,
wakati akizungumza na Chama cha Wanawake Wachimbaji wa Madini Tanzania
(TAWOMA).
Mbibo
amesema wanawake wanazidi kushiriki si tu kwenye uchimbaji mdogo, bali pia
kwenye biashara, uongezaji thamani, teknolojia na kutoa huduma katika Sekta ya
Madini.
“Kwa sasa
tunaona mabadiliko makubwa. Wanawake wanashiriki kwenye nyanja zote za mnyororo
wa madini, kutoka migodini hadi sokoni. Wizara ya Madini inajivunia kuwa mfano
bora wa usawa wa kijinsia nchini,” amesema Mbibo.
Aidha,
Mbibo ameongeza kuwa, Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi
yanayojumuisha utoaji wa leseni, upatikanaji wa maeneo ya uchimbaji na mafunzo
ya kitaalamu, hatua zinazowezesha wanawake kushiriki kwa ufanisi sambamba na
wanaume.
“Hatuwezi
kuacha kundi kubwa la wananchi nyuma. Wanawake wana mchango mkubwa wa kuleta
mageuzi katika sekta ya madini na Wizara itaendelea kusimama bega kwa bega
nao,” amesisitiza Mbibo.
Kwa
upande wake Katibu Mkuu wa TAWOMA Salma Ernest
amesema hatua zinazozoendelea kuchukuliwa Serikali zimekuwa chachu ya
mafanikio kwa wanawake wengi waliokuwa wakikosa nafasi katika sekta hiyo.
Amesisitiza
kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Madini imeendelea kutoa kipaumbele kwa
wanawake kwa kuwapatia vitalu vya uchimbaji na kuwasaidia kupata elimu ya
kitaalamu.
“Kuongezeka
kwa idadi ya wanawake sekta ya madini si tu kunawanufaisha wao binafsi, bali
pia kunachangia ustawi wa familia na jamii kwa ujumla” amesema Salma.
Kwa
kuongezeka kwa idadi ya wanawake katika Sekta ya Madini, Tanzania inajiweka
katika nafasi bora zaidi ya kuendeleza uchumi jumuishi unaozingatia usawa, huku
dhana ya “Madini ni Maisha na Utajiri” ikipata tafsiri ya vitendo.




0 Maoni