TANAPA yafanikisha Kijiji cha Kalalani kuwa na Kituo cha Polisi

 

Shangwe! Furaha! Nderemo na Vifijo vilirindima katika kijiji cha Kalalani baada ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) chini ya Mwenyekiti wake wa Bodi ya Wadhamini - Mkuu wa Majeshi (Mstaafu) Jenerali George Waitara alipokabidhi Kituo kipya cha Polisi - Kalalani ili kuimarisha ulinzi wa wananchi na mali zao.

Ujenzi wa Kituo hicho uligharimu kiasi cha shilingi takribani milioni 150.62 ikihusisha jengo lenye vyumba zaidi ya 8, eneo la mapokezi, mifumo ya maji safi na maji taka pamoja na mifumo ya umeme ikiwa ni utamaduni wa TANAPA kurudisha faida ya uhifadhi na utalii kwa jamii zinazozunguka Hifadhi za Taifa nchini ili washiriki katika ulinzi wa maliasili.

Hata hivyo, Kituo cha Polisi Kalalani kitakuwa ni mwarobani wa kero zote za kiusalama ambazo wananchi hao walikuwa wakizifuata umbali wa zaidi ya kilometa 30 hususani katika kijiji cha Masewa.

Akikabidhi mradi huo kwa Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Kamishna wa Uhifadhi (Mstaafu) Mhe. William Mwakilema kwa niaba ya wananchi hao, Jen. Waitara alisema;

“Ujenzi wa kituo hiki ni muhimu sana ukizingatia kijiji hiki cha Kalalani kiko mpakani mwa nchi, hivyo matarajio ya ulinzi na usalama ni mkubwa, hivyo niwaase wanakijiji wa Kalalani na vijiji vya jirani kufanya kazi kwa ukaribu na Jeshi la Polisi watakaotumia kituo hiki.”

Akikata utepe wakati wa makabidhiano ya kituo hicho kuashiria kufunguliwa kwake, Mhe. Mwakilema alisema, “Niwasisitize wananchi wa Kata ya Kalalani, jengo hili licha ya sababu za kiusalama pia ni pamoja na kuimarisha ulinzi wa hifadhi yetu ya Mkomazi.”

Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Polisi Joseph Ng’weve akimwakilisha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga aliwashukuru TANAPA kwa msaada huo alisema kuwa kituo hicho kitakuwa mkombozi kwa wananchi wa Kalalani na maeneo ya jirani ambayo kwa muda mrefu yalikosa huduma ya karibu ya ulinzi wa polisi.

Naye, Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji cha Kalalani Orolonyo Tulakani alisema kuwa wamepokea mradi huo kwa furaha na matumaini makubwa kwani utasaidia kupunguza matukio ya uhalifu na kuongeza amani.

Makabidhiano hayo yanaashiria ushirikiano na mshikamano kati ya majeshi haya mawili katika kusimamia ulinzi na usalama wa wananchi na mali zao kwa ajili ya maendeleo endelevu.

Hafla ya uzinduzi wa Kituo hicho cha Polisi Kalalani ilifanyika leo Septemba 22, 2025 Katika kijiji cha Kalalani katika Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga ambapo wanakijiji hao walitoa Ekari 3 za  ardhi kwa ajili ya ujenzi wa Mradi huo.




Na. Jacob Kasiri - Tanga.

Chapisha Maoni

0 Maoni