Mgombea
urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM),
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kujenga Kampasi ya Chuo cha Uhasibu
Arusha (IAA) katika mkoa wa Ruvuma, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha
elimu ya juu nchini.
Dkt.
Samia ametoa ahadi hiyo leo wakati akijinadi mbele ya maelfu ya wananchi
waliojitokeza katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye viwanja vya Chuo cha
Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) mjini Songea, mkoani Ruvuma.
Amesema
kuwa hatua hiyo inalenga kuongeza fursa za elimu ya juu kwa vijana wa mkoa huo
na kanda nzima ya kusini, pamoja na kuandaa wataalamu wa masuala ya fedha,
biashara na usimamizi wa rasilimali kwa kiwango cha kitaifa na kimataifa.
“Kampasi
hii ya Chuo cha Uhasibu Arusha itakapokamilika, itakuwa na uwezo wa kuchukua
wanafunzi zaidi ya 10,000 kwa wakati mmoja. Nawaambia wana Ruvuma: jiandaeni
kuwa wahasibu wa baadaye,” alisema Rais Samia huku akishangiliwa na umati wa
watu.
Rais
Samia, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, amesema serikali ya chama hicho
itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya elimu na kuongeza vyuo vikuu na vya
kati katika maeneo mbalimbali nchini, ili kuhakikisha elimu inawafikia wananchi
wote bila ubaguzi wa kijiografia.
0 Maoni