Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Tanga imefanikiwa
kuokoa kiasi cha shilingi milioni 10.5 baada ya kufuatilia kwa karibu
utekelezaji wa mradi wa barabara ya kiwango cha lami katika Halmashauri ya
Wilaya ya Muheza, ikiwa ni sehemu ya miradi ya maendeleo ya sekta ya barabara.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Tanga, Mkuu wa TAKUKURU mkoa huo, Ramadhani
Ndwatah, alisema kuwa fedha hizo ziliokolewa baada ya kubainika kuwepo kwa
upungufu wa nguzo tatu za taa za umeme wa jua kwenye barabara yenye urefu wa
mita 830, ambayo ilipaswa kuwa na nguzo 29 lakini ziliwekwa 26 tu.
“Huu ni
mfano halisi wa namna taasisi yetu inavyotekeleza wajibu wa kuhakikisha fedha
za umma zinatumika ipasavyo,” alieleza Ndwatah na kuongeza kuwa hatua stahiki
zilichukuliwa mara moja kwa kuwasiliana na TARURA (W) ili kuhakikisha kasoro
hizo zinatekelezwa kwa haraka.
Ndwatah
aliongeza kuwa hatua hiyo ilisaidia kurejeshwa kwa nguzo hizo tatu zenye
thamani ya Shilingi milioni 10.5, zilizowekwa kwa viwango stahiki kulingana na
mkataba na BOQ ya mradi husika. Alisisitiza kuwa hilo ni jukumu muhimu la
TAKUKURU katika kuzuia upotevu wa rasilimali za taifa.
Aidha,
katika kipindi cha Aprili hadi Juni 2025, TAKUKURU Tanga ilifuatilia miradi 29
ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 7.9, ambapo miradi 10
kati ya hiyo yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 2.8 ilibainika kuwa na
changamoto mbalimbali za kiutekelezaji.
“Baadhi ya
miradi haikulipiwa VAT, mingine haikufuata michoro rasmi au kucheleweshwa
kinyume cha mikataba,” alisema Ndwatah huku akibainisha kuwa mamlaka husika
zimejulishwa kwa hatua za kiutawala na kisheria kuchukuliwa.
Kwa mujibu
wa Ndwatah, TAKUKURU itaendelea kufuatilia kwa karibu matumizi ya fedha katika
miradi ya maendeleo, huku pia ikitilia mkazo elimu kwa umma kuelekea uchaguzi
mkuu wa 2025.
0 Maoni