Tafiti
zinaonesha kuwa, zaidi ya asilimia 70 ya ubunifu mpya wa teknolojia duniani
unahusishwa moja kwa moja na taaluma ya uhandisi ambayo ndani yake hujumuisha
masuala mbalimbali ikiwemo Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA),
Nishati, viwanda na akili mnemba.
Hayo
yamebainishwa Septemba 25, 2025 jijini Dar es Jijini Dar es Salaam na Naibu
Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko alipomwakilisha Waziri
Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa kufungua Maadhimisho ya 22 ya Siku ya
Waandisi kwa Mwaka 2025.
Amesema
kuwa Serikali inawahitaji na kuwategemea wahandisi nchini ambao wana fursa ya
kuchangia maendeleo ya nchi kupitia utekekezaji wa majukumu yao.
Dkt.
Biteko ameongeza kuwa zaidi ya asilimia 90 ya uvumbuzi na maendeleo ya viwanda
huhitaji huduma ya wahandisi moja kwa moja.
“Kwa
niaba ya Serikali naomba niwakumbushe kuwa taifa linawategemea sana.
Tunawategemea, tunawahitaji naomba mjue Serikali itaendelea kuwategemea wakati
wote mnapotekeleza majukumu yenu,” amesema Dkt. Biteko.
Amefafanua
kuwa wahandisi hufanya shughuli za ubunifu na uundaji, utafiti na uvumbuzi,
usimamizi wa miradi, uhakiki wa usalama na ubora pamoja na ushauri wa Sera na
ubunifu wa mifumo mbalimbali duniani kote. Hivyo ni muhimu wajitahidi kuakisi
na kutafsiri matarajio yaliyomo katika mioyo ya jamii na kuyaweka katika
uhalisia.
Aidha,
Dkt. Biteko ameitaka ERB kuwasaidia wahandisi nchini kwa kuwaelekeza na kuwapa
mootisha pale wanapofanya vizuri badala ya kubaki kuwa tishio kwao na kuwapa
adhabu baada ya kukosea.
Ameendelea
kusema motisha kwa wahandisi wazawa
walioshiriki katika ujenzi wa miradi ya kimkakati nchini sambamba na kuwapa
hamasa na kuwajengea uwezo wa kushiriki miradi mingine ya kimkakati ni muhimu
ili kuwapata wahandisi wazalendo.
Naye,
Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega amesema kuwa Wizara itaendelea kuimarisha
mazingira ya taaluma ya uhandisi ikiwa ni pamoja na kuruhusu mafunzo ya
kuongeza viwango vya taaluma hiyo.
Amebainisha
kuwa Wizara inaendelea kuhakikisha wahandisi wazawa wanashiriki kikamilifu
katika miradi ya kimkakati kama vile SGR. Aidha, ameishukuru Serikali Serikali
inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan kwa kuendelea kujenga miradi ya maendeleo nchini.
Kwa
upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Mhe. Albert Msando akizungumza kwa niaba
ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam amewaasa
wahandisi hao kusimamia taaluma yao katika kutekeleza majukumu yao.
Mwenyekiti
wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), Mhandisi Menye Manga amesema katika Dira
ya Taifa ya Maendeleo 2025 imetekeleza miradi mikubwa ikiwemo daraja la Kigongo
Busis na wahandisi wengi wa wazawa wameshiriki katika kujenga tofauti na
ilivyokuwa awali.
Kaimu
Msajili wa Bodi ya Usajili wa Waandisi (ERB), Wakili Mercy Jilala amesema kuwa
hadi kufikia mwaka 2025 ERB imesajili zaidi ya wahandisi 44,000.
ERB
inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuwezesha usajili zaidi wa
wahandisi hususan wanawake.
Aidha,
mkutano huo pia umehudhuriwa na washiriki kutoka nchi za Uganda, Kenya,
Ethiopia na India.
Sambamba
na maadhimisho ya mwaka 2025 zaidi ya washiriki 4,448 wamehudhuria mkutano huo
na wahandisi 400 wamekula kiapo cha maadili ya taaluma hii ya uhandisi.
Na. Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati




0 Maoni