Serikali imetangaza kukamilika kwa maandalizi ya Mpango Elekezi wa Muda Mrefu wa Maendeleo (Long-Term Perspective Plan – LTPP), hatua muhimu inayofungua njia kwa kuanza kwa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Akizungumza
leo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dk. Kitila Mkumbo,
alisema kuwa Serikali tayari imeunda Timu ya Wataalam 22 kutoka sekta ya umma
na binafsi kwa ajili ya kuandaa Mpango wa Nne wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka
Mitano (FYDP IV), ambao ulianza kutekelezwa rasmi kuanzia Julai 1, 2025.
“Timu hii
ya wataalam, inayoongozwa na Dk. John Mduma, itakuwa na jukumu la kuibua na
kupendekeza miradi ya kielelezo na kimkakati itakayotekelezwa ndani ya miaka
mitano ijayo,” alisema Dk. Mkumbo.
Miradi Mikubwa Kuendelezwa
Katika
mapendekezo ya awali, timu hiyo imependekeza kuendeleza miradi 12 kati ya 17 ya
kielelezo iliyoibuliwa chini ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano
(FYDP III) 2021/22 – 2025/26.
Miradi
mitatu kati ya hiyo imekamilika tayari, ikiwemo:
- Mradi wa Kufua Umeme wa
Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) unaozalisha megawati 2,115
- Ujenzi wa madaraja makubwa
na madaraja ya juu (flyovers) 13
- Kiwanda cha Sukari cha
Mkulazi
Miradi
mingine iliyopendekezwa kuendelezwa katika FYDP IV ni:
- Mradi wa Reli ya Kisasa ya
SGR,
wenye vipande vinane
- Mradi wa Bomba la Mafuta
Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga (Tanzania),
ambao umefikia asilimia 55
- Bandari ya Uvuvi Kilwa
Masoko na ununuzi wa meli, ambao umefikia asilimia 75
- Mradi wa Kufua Umeme wa
Ruhudji (MW 358) –
umefikia asilimia 6
- Mradi wa Kufua Umeme wa
Rumakali (MW 222) – umefikia asilimia 7
- Mradi wa Gesi Asilia (LNG) –
Lindi –
umefikia asilimia 6
- Utafiti wa Mafuta na Gesi
katika Kitalu cha Eyasi-Wembere (Manyara) – umefikia asilimia 5
- Utafiti wa Mafuta na Gesi
Mnazi Bay – Mtwara – umefikia asilimia 6
- Mradi wa Magadi Soda
Engaruka – Arusha – umefikia asilimia 5
- Uendelezaji wa Kanda Maalum
ya Kiuchumi – Bagamoyo Eco Maritime City – umefikia asilimia 5
- Reli ya Kusini (Mtwara –
Mbamba Bay, na matawi ya Liganga na Mchuchuma) – hatua za awali
- Mradi wa Makaa ya Mawe
Mchuchuma na Chuma Liganga – umefikia asilimia 6
Mchuchuma na Liganga Kufufuliwa Upya
Akizungumzia
kwa kina mradi wa Mchuchuma na Liganga, Dk. Mkumbo alisema kuwa mradi huo ni wa
kimkakati kwa maendeleo ya sekta ya viwanda, ukiwa miongoni mwa miradi ya
kimageuzi ndani ya Dira 2050.
“Makaa ya
mawe yatatumika kuzalisha umeme kwa ajili ya viwanda, huku chuma kikitarajiwa
kuwa malighafi ya msingi kwa sekta ya ujenzi na viwanda. Kukamilika kwa mradi
huu kutaiweka Tanzania kwenye nafasi ya nne Afrika kwa uzalishaji wa chuma,”
alifafanua.
Historia
ya mradi huo inaanzia mwaka 1996, wakati Baraza la Mawaziri lilipoamua
utekelezaji wake kupitia Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC). Mwaka 2011, NDC
iliingia ubia na Kampuni ya Sichuan Hongda Corporation (SHG) ya China na kuunda
kampuni ya TCIMRL, ambapo NDC ilimiliki asilimia 20 na SHG asilimia 80.
Mwaka
2015, utekelezaji wa mradi ulisimamishwa baada ya Serikali kubaini kuwa baadhi
ya vipengele vya mkataba havakulinda maslahi ya taifa. Kufuatia hali hiyo,
Serikali iliunda Timu Maalum ya Majadiliano mwaka 2017, lakini mpaka mwaka 2020
hakuna mwafaka uliofikiwa.
Hata
hivyo, matumaini mapya yameibuka baada ya SHG kununuliwa na kampuni ya Shudao
Investment Group (SDIG) mwaka 2024. Tangu Januari 2025, Serikali imekuwa
ikijadiliana na SDIG kuhusu mkataba mpya, na kwa mujibu wa Dk. Mkumbo,
mazungumzo yapo hatua za mwisho.
“Tayari
fidia imelipwa kwa wananchi katika eneo la mradi, na eneo hilo sasa
linamilikiwa rasmi na Serikali,” aliongeza.
Mazingira Bora ya Biashara
Kama
sehemu ya maandalizi ya utekelezaji wa Dira 2050 na FYDP IV, Serikali
inaendelea kupitia Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji
(MKUMBI). Lengo kuu ni kuvutia wawekezaji wa ndani na nje kwa kuweka
mazingira rafiki kwa biashara na uwekezaji.
Dk.
Mkumbo alisisitiza kuwa mafanikio ya Dira 2050 yatategemea sana ushiriki wa
sekta binafsi. Kwa mujibu wake, Serikali imejipanga kuijengea uwezo sekta
binafsi, hasa biashara ndogo na za kati, kwa kuwasaidia kwa mitaji, maarifa na
miundombinu ili waweze kushindana katika soko la kikanda na kimataifa.
“Katika
Dira 2050, nafasi ya sekta binafsi ni ya msingi. Serikali itaendelea kuweka
mazingira ya kuwavutia wawekezaji kutoka kila pembe ya dunia,” alisema Dk.
Mkumbo.

0 Maoni