Maabara
ya Tume ya Madini imevuka lengo la upimaji sampuli za madini kwa mwaka wa fedha
ulioisha Juni 30, 2024/2025, baada ya kupima jumla ya sampuli 7684 dhidi ya
lengo la 6,800.
Hili ni
ongezeko linaloashiria ufanisi mkubwa wa maabara katika kutoa huduma kwa
wachimbaji na wafanyabiashara wa madini.
Akizungumza
katika Maonesho ya Nane ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini mkoani Geita,
Mkemia kutoka maabara hiyo, David
Lyandala amesema maabara inaendelea kutoa huduma za kitaalam za uchunguzi wa
madini ili kubaini ubora na kiasi kilichomo.
Huduma
hizo zinajumuisha uchunguzi wa dhahabu, makinikia, kaboni, kimiminika chenye
dhahabu, mbale za udongo na miamba kwa kutumia (Fire Assay), pamoja na
uchunguzi wa metali kama shaba, chuma, nikeli, manganizi, galena na zinki kwa
kutumia mashine za kisasa za X-Ray Fluorescence (XRF).
Aidha,
maabara hupima madini ya kinywe (graphite), unyevunyevu wa udongo na miamba,
pamoja na upotevu wa uzito kwa kuchoma (Loss in Ignition).
Lyandala
ameongeza kuwa vifaa vya kisasa kama XRF Machine, Atomic Absorption
Spectrometer (AAS), CNHS Analyzer na furnaces vimeongeza ufanisi wa huduma,
huku akitoa elimu kwa wadau kuhusu umuhimu wa kupima sampuli kabla ya kufanya
maamuzi ya kibiashara.
Kwa
upande wake, mchimbaji mdogo kutoka Geita, John Magesa, amesema huduma hizo
zimekuwa msaada mkubwa kwa wachimbaji wadogo.
“Zamani tulikuwa tunauza madini bila kujua ubora
wake, jambo lililotufanya kupoteza thamani. Sasa tunapata uhakika na tunaweza
kufanya biashara yenye faida,” amesema.
Maabara
ya Tume ya Madini ipo TIRDO Complex, Kimweri Avenue, Msasani, Dar es Salaam, na
inatoa huduma kwa wachimbaji na wafanyabiashara
wa madini kote nchini.




0 Maoni