WAZIRI
MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali itaendelea kufanya uwekezaji wa
kutosha ili kuhakikisha Watanzania wanapata huduma Bora za magonjwa ya moyo na
mishipa.
Amesema
kuwa uwekezaji huo unaenda sambamba na dhamira ya kuendelea kupunguza gharama
za matibabu hayo kwa kwenda nje ya nchi hivyo kusaidia kuokoa maisha ya Watanzania.
Amesema
hayo leo Jumapili (Septemba 28, 2025) alipokuwa mgeni rasmi katika mbio za
hisani za Saifee Marathon zilizoanzia na kuishia katika viwanja vya green park
Oysterbay, jijini Dar es Salaam.
Amesema
kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
imewekeza katika ununuzi wa vifaa vya kisasa vya kutoa huduma za uchunguzi
ikiwemo ECHO, ECG, Ultrasound na Holter.
Amesema
kuwa takwimu za Shirika la Afya duniani zinaonesha kuwa takribani asilimia 71
ya vifo vyote duniani vinasababishwa na magonjwa yasiyoambukiza.
"Inakadiriwa kuwa zaidi ya watu milioni 4.9 wenye umri wa kuanzia miaka 30
hadi 79 wanamatatizo ya moyo na mishipa ya damu".
"Ndugu
wananchi nendeni mkafanye uchunguzi ili muwe na uhakika wa afya zenu, zamani
huduma hizi ililazimu kusafiri kwenda kwenye nchi kama India, Uingereza na
Ujerumani lakini kwasasa tiba hizi ziko hapahapa nchini".
Aidha,
Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa kushirikiana na wadau wote wa afya kwenye
kutoa elimu ya jamii kuhusu namna ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza kwa
kuwa yamethibitishwa kwamba ni hatari.
"Sisi
wananchi tunaowajibu wa kuhakikisha tunafanya uchunguzi wa afya zetu mara kwa
mara kwani kugundua tatizo mapema huwezesha matibabu kwa wakati na kuokoa
maisha".
Kwa
upande wake, Mkurugenzi Mtendaji WA Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Peter Kisenge amesema kuwa Serikali inaendelea kutekeleza sera ya afya ya
mwaka 2007 ikilenga kuboresha huduma za magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo
shinikizo la juu la damu " Huduma hizi zinatolewa katika ngazi zote za
vituo vya huduma za afya".
Ameongeza
kuwa, nchini Tanzania takwimu zinaonesha kuwepo kwa ongezeko la wagonjwa wa
shinikizo la damu kutoka wagonjwa milioni 1.73 mwaka 2023/2024 hadi wagonjwa
milioni 1.77 mwaka 2024/2025 Sawa na ongezeko la asilimia 98.
Awali,
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Saifee Murtaza Alibhai amesema kuwa dhamira
ya mbio hizo hazijaishia kukimbia pekee, bali zinalenga kuelimisha jamii na
kusisitiza kinga ya afya.
Ameongeza
kuwa mikakati ya hospitali hiyo inaunga mkono Dira ya Taifa ya Maendeleo ya
mwaka 2050 inayosisitiza maendeleo ya watu. "Tunajivunia na kumuunga Mkono
Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ukuaji wa sekta ya afya
nchini".
Lengo la
marathon hizo ni kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kuchukua hatua za
kujikinga na magonjwa ya moyo na mishipa ya damu kwa kutoa elimu ya afya kwa
wananchi kuhusu mtindo bora wa maisha.
Lengo
lingine ni kuimarisha uchunguzi wa mapema wa magonjwa yasiyoambukiza, pamoja na
kuhimiza ushirikiano wa wadau mbalimbali katika mapambano dhidi ya
magonjwa yasiyoambukiza.




0 Maoni