Makuyuni Wildlife Park ni hifadhi ya kimkakati - Dkt. Abbasi

 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, amesema Hifadhi ya Wanyamapori Makuyuni inayojulikana kama Makuyuni Wildlife Park ni hifadhi mpya ya kimkakati, inayofikika kwa urahisi na inayompa fursa mtalii wa kuona wanyamapori kwa ukaribu zaidi na kwa muda mfupi.

Dkt. Abbasi ameyasema hayo leo Septemba 28,2025, alipotembelea Hifadhi ya Wanyamapori Makuyuni ikiwa ni muendelezo wa ziara ya kikazi katika maeneo yanayosimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA).

Aidha, Dkt. Abbasi ameongeza kuwa kutokana na upekee wa Hifadhi hii, amesisitiza kuendelea kubuniwa kwa mazao mengi ya utalii ili kumpa mtalii fursa ya kufanya shughuli mbalimbali za utalii akiwa ndani ya hifadhi.

Kwa upande wake, Kaimu Kamishna wa Uhifadhi - TAWA, Mlage Yussuf Kabange amesema kuwa, TAWA imeboresha miundombinu iliyopo katika Hifadhi ya Wanyamapori Makuyuni, ikiwemo ujenzi wa bwawa la kukusanyia maji kwa ajili ya wanyamapori, ujenzi wa barabara na vivuko vinavyoifanya hifadhi iweze kufikika katika majira yote ya mwaka.

Sambamba na hilo, Kamishna Kabange amesema kuwa TAWA inaendelea na jitihada za kutangaza utalii na kuvutia wawekezaji ili wawekeze katika maeneo mbalimbali yanayosimamiwa na TAWA.

Awali, akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa Makuyuni Wildlife Park, Afisa Mhifadhi Ruahamangi Kishe, amesema Hifadhi ya Makuyuni imesheheni vivutio mbalimbali wakiwemo wanyamapori kama vile Tembo, Simba, Twiga, Choroa, Pundamilia, Nyati na Pofu. Pia hifadhi ya Makuyuni imezungukwa na jamii ya kimasai inayotoa fursa ya kufanya utalii wa kiutamaduni.

Makuyuni Wildlife Park inapatikana Wilaya ya Monduli, takribani kilometa 40 kutoka Arusha Mjini.


               Na. Joyce Ndunguru, Arusha.

Chapisha Maoni

0 Maoni