Ujenzi wa
daraja la mawe katika Mto Katupa sambamba na barabara ya changarawe ya
Majimoto-Namanyele katika Halmashauri ya Mpimbwe, mkoani Katavi, umetajwa kuwa
mkombozi kwa wakulima wa eneo hilo, kwa kuongeza tija katika kilimo na
kuchochea uchumi wa wananchi.
Akizungumza
wakati wa ukaguzi wa miradi hiyo, Meneja wa Wakala ya Barabara za Vijijini na
Mijini (TARURA) Wilaya ya Mlele, Mhandisi Paul Mabaya alisema kuwa mradi huo
unatekelezwa kwa gharama ya shilingi milioni 361.95 na hadi sasa umefikia
asilimia 95 ya utekelezaji.
"Mradi
huu unajumuisha ujenzi wa daraja la mawe, barabara ya changarawe yenye urefu wa
kilomita 1.5 pamoja na kalvati tatu. Fedha za mradi huu zinatokana na ufadhili
wa Benki ya Dunia kupitia mradi wa RISE," alisema Mhandisi Mabaya.
Aliongeza
kuwa utekelezaji wa miradi hiyo unalenga kuboresha upatikanaji wa huduma muhimu
kwa wananchi, hasa katika maeneo ya vijijini ambako shughuli za kilimo ndio
mhimili mkuu wa uchumi wa wananchi.
Kwa
upande wake, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2025, Ndugu
Ismail Ali Ussi, alieleza kuwa serikali itaendelea kuhakikisha wananchi wake
wanapata miundombinu bora ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli
za maendeleo.
"Serikali
kupitia miradi kama hii, inalenga kuweka mazingira wezeshi kwa wananchi wake.
Hii ndiyo dhamira ya dhati ya kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma katika
maendeleo," alisema Ussi.
Naye
mkazi wa kijiji cha Majimoto, Shija Shigela, licha ya kuipongeza TARURA kwa
ujenzi wa daraja na barabara hiyo, aliiomba mamlaka hiyo kuendelea na jitihada
hizo kwa kujenga miradi mingine zaidi ya barabara vijijini.
"Miradi
hii inatufungulia fursa nyingi, hasa sisi wakulima. Tunaiomba serikali na
TARURA waendelee kutuunga mkono kwa kuboresha zaidi miundombinu ya barabara
maeneo ya vijijini," alisema Shigela.
Miradi
hii ni miongoni mwa hatua zinazochukuliwa na serikali katika kuhakikisha kuwa
miundombinu ya usafiri vijijini inaimarika, ikiwa ni sehemu ya jitihada za
kupunguza umaskini na kuharakisha maendeleo ya wananchi katika ngazi ya chini.



0 Maoni