Mkuu wa Mkoa wa Arusha CPA Amos
Makalla leo Septemba 21, 2025 ametembelea na kufanya Kikao Kazi na Menejimenti
ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) katika Hifadhi ya Taifa Ziwa
Manyara iliyopo Mto wa Mbu mkoani Arusha.
Katika kikao chake na Menejimenti
ya TANAPA Mhe. Makalla alipokea taarifa ya jumla ya Shirika kutoka kwa Kamishna
wa Uhifadhi - TANAPA pamoja na kufanyiwa mawasilisho ya utendaji kazi kutoka
kwa Wakuu wa Hifadhi ya Taifa Arusha na Ziwa Manyara ambazo zipo mkoani Arusha
na kuipongeza TANAPA kwa kuendelea kusimamia vema shughuli za Uhifadhi na
Utalii katika maeneo yote ya Hifadhi za Taifa hapa nchini.
"Niwapongeze sana kwa
kusimamia maeneo haya ya Uhifadhi. TANAPA mna dhamana kubwa ya kuendeleza
Uhifadhi na Utalii wa nchi yetu kwa kuvilinda na kuviendeleza vivutio na
rasilimali tulizojaaliwa na Mwenyezi Mungu katika nchi yetu. Niwahakikishie
mtapata ushirikiano mkubwa kutoka kwangu.
"Hifadhi za Taifa ni maeneo
yaliyotengwa kisheria na mipaka yake inajulikana. Kuharibika kwa maeneo haya mliyokasimiwa
kuyasimamia kwa niaba ya watanzania ni jambo ambalo halipaswi kutokea kwani
mara nyingi kunasababishwa na watu wengine wasio na mapenzi mema kutanguliza
ubinafsi mbele. Hakikisheni mnafanya kila jitihada kuendeleza Uhifadhi kwani
Utalii ni matokeo ya Uhifadhi. Mtalii atakuja kuona nini kama
hujahifadhi?" alisema Mhe. Makalla.
Naye, Kamishna wa Uhifadhi
TANAPA CPA Musa Nassoro Kuji alibainisha
kuwa TANAPA imejidhatiti vilivyo katika kulinda na kuendeleza rasilimali zote
zilizopo katika Hifadhi za Taifa na kuongeza kuwa TANAPA itaendelea kutoa mchango mkubwa katika
maendeleo ya Taifa.
Aidha, Kamishna Kuji aliongeza
kuwa katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Dkt.
Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, TANAPA
imeshuhudia idadi kubwa ya wageni katika maeneo yote yanayosimamiwa na Shirika.
Pongezi zetu zimfikie Mhe. Rais
Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani kupitia filamu ya "Tanzania: The Royal
Tour" na ile ya "Amazing Tanzania" zimeleta mapinduzi makubwa
katika sekta ya utalii nchini ambapo kwa hali ilivyo sasa ni vigumu
kutofautisha kati ya "High season" na "Low season" kwani
tunashuhudia idadi kubwa ya watalii katika
vivutio vyetu".
Mhe. CPA Amos Makalla yupo kwenye
ziara ya kikazi katika taasisi na maeneo mbalimbali mkoani Arusha ikiwa ni
sehemu ya kukutana na wadau pamoja na kuwatia moyo watumishi na wananchi ili
kila mmoja ajione kuwa anayo nafasi katika kuchangia uchumi wa Mkoa wa Arusha
na Taifa kwa ujumla.
Na. Edmund Salaho - Hifadhi ya
Taifa Ziwa Manyara
0 Maoni