WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa
amesema kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatambua kwa dhati
mchango wa madhehebu ya dini ikiwemo BAKWATA na wadau wote wa elimu katika
kuimarisha maadili, kuendeleza maarifa na kuleta mshikamano wa kitaifa kupitia
elimu.
Amesema kuwa elimu haiwezi
kukamilika kama hakuna maadili kwani ndiyo yanayojenga utu, heshima na
mshikamano wa kijamii. "Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa mstari wa mbele
kuhakikisha elimu inakuza maarifa na ujuzi, sambamba na malezi yanayoimarisha
tabia bora na maadili ya kizalendo kwa vijana wa Kitanzania".
Amesema hayo Jumamosi Septemba
20, 2025 alipomwakilisha Rais Dkt. Samia katika hafla ya usiku ya utoaji tuzo
za elimu za mufti iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Serena hotel jijini
Dar es Salaam.
"Rais Dkt. Samia
anawapongeza sana BAKWATA kwa juhudi kubwa mnazozifanya katika masuala yote ya
maendeleo ya jamii hususan mchango wenu katika kuendeleza elimu na kuimarisha
mshikamano wa kitaifa kupitia malezi ya maadili na maarifa, Serikali inathamini
sana mchango wa taasisi za dini kama BAKWATA katika kuunga mkono malezi ya
watoto na vijana". Amesema Mheshimiwa Majaliwa.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa
Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) limekuwa na mchango mkubwa katika
kukuza sekta ya elimu nchini kwani limeanzisha na kuendesha shule, madrasa na
vyuo vinavyotoa elimu bora ya dini na ya kawaida, sambamba na kujenga maadili
mema kwa vijana.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amesema
kuwa Tuzo za Elimu za Mufti ni jukwaa la kitaifa la kutambua na kuthamini
michango ya kipekee katika elimu, ubunifu, malezi na maadili ya vijana wa
Kitanzania. "Tukio hili linaakisi muonekano wa taifa lenye watu
wanaojituma, wanaothamini elimu, na wanaochangia ustawi wa taifa letu bila
kujali itikadi za dini au misimamo ya kisiasa."
Amesema kuwa tuzo hizo zinatambua
ubunifu, uongozi, mshikamano wa jamii na mchango wa wadau katika kuhakikisha
elimu inakuwa jumuishi, bora na endelevu. Hili ni tukio linaloonesha kwa
vitendo methali ya Mtume (S.A.W) isemayo: “tafuteni elimu hata kama ni mpaka
China”; ikiashiria kuwa elimu ni chombo cha ukombozi na maendeleo ya jamii
yoyote na hakuna mipaka katika kuitafuta."
Amesema Serikali kwa upande wake
kupitia Dira ya Maendeleo ya 2050 imeweka malengo ya muda mrefu kuhakikisha
kwamba itaendeleza ushirikiano kati ya taasisi za dini, sekta binafsi na
mashirika ya kimataifa ili kuhakikisha elimu inaendelea kuwa injini ya
maendeleo ya taifa.
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa
ametoa wito kwa sekta binafsi, mashirika ya kidini, mashirika ya maendeleo na
jamii kwa ujumla kuwekeza zaidi katika elimu. "lengo ni kuhakikisha kuwa
tunawajenga vijana wetu wawe wabunifu, waadilifu na wazalishaji wa fursa za
ajira badala ya watafuta ajira pekee, ongezeni uwekezaji katika elimu".
Kwa upande wake Mufti na Sheikh
Mkuu wa Tanzania Dkt. Abubakar Zubeir bin Ally, amesema kuwa tuzo hizo
zimetolewa kutokana na bakwata kuthamini elimu kwa kuwa uislam ni elimu sio
ujinga "Elimu ndio uhai wa uislam na ni nguzo kuu ya uslam, uislam unamchango
mkubwa sana duniani katika elimu."
Kadhalika, Sheikh Dkt. Abubakar
amempongeza Rais Dkt. Samia kwa usimamizi wake mzuri kwa namna anavyosimamia
elimu nchini. Pamoja na hii pia tunathamini sana wadau mbalimbali wanaojitoa
katika kusimamia sekta ya elimu na kutilia mkazo masuala ya elimu."
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa
elimu wa Bakwata Ally Abdalah Ally amesema kuwa mpango wa tuzo hizo
zilizobuniwa na Mheshimiwa Mufti zinalengo la kuinua na kuwatia moyo wadau wa
elimu wanaojitoa na kujitolea ipasavyo katika mabadiliko chanya ya elimu kwa
maendeleo endelevu. Katika hafla hiyo, tuzo ishirini na tatu zilitolewa.
0 Maoni