Mgombea Ubunge wa Jimbo la
Bukombe kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Ndugu. Doto Mashaka Biteko
amewapongeza wananchi wa Kata ya Bugelenga, Wilaya ya Bukombe kwa kushirikiana
na kufanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Kata yao
ikiwemo ujenzi wa shule, barabara na miradi ya maji.
Ametaja moja ya mradi kuwa ni
ujenzi barabara ya Bufanka - Ikalanga hadi Bukombe ambapo ameahidi kuwa CCM
ikipewa dhamana ya kuongoza kwa kipindi kingine cha miaka mitano, itatekeleza
miradi zaidi ili kuwaletea maendeleo wananchi kwa kukabiliana na kero
zinazowakabili.
Dkt. Biteko amesema hayo Septemba
20, 2025 wakati wa mkutano wa kampeni katika Kata ya Bugelenga wilayani Bukombe
mkoani Geita ikiwa ni sehemu Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na
Madiwani utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.
Amesema katika kipindi cha miaka
mitano iliyopita, Serikali imefikisha umeme katika vijiji vyote nchini vikiwemo
vijiji sita vya Kata ya Bugelenga na kazi iliyobaki ni kupeleka umeme katika
vitongoji tisa vya Kata hiyo.
Amewaeleza wananchi kuwa CCM
itaendelea kusogeza huduma bora za jamii ambapo ameahidi kuwa kuanzia sasa
wananchi wakiunganisha umeme watapewa majiko ya umeme bure ikiwa ni njia ya
kupunguza gharama ya kupikia ikilinganishwa na matumizi ya kuni.
Dkt. Biteko pia amesema watajenga
kituo kikubwa cha kupooza umeme ili kuweza kusambaza umeme huo hadi Mbogwe,
watajenga madarasa, maabara na jengo la utawala.
“ Mgombea udiwani ameeleza kuhusu
shule zinazohitaji ukarabati hivyo ni lazima zikarabatiwe katika kipindi
kinachokuja. Pia, Nataka niwaambie tutajenga wodi kwa ajili ya kulaza wagonjwa
katika Kata hii,” amesema Dkt. Biteko.
Aidha, Dkt. Biteko amesema katika
kipindi cha miaka mitano ijayo CCM imedhamiria kusogeza huduma kwa wananchi kwa
kuongeza miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa maji.
Kuhusu umuhimu wa elimu, amewaasa
wananchi hao kuwasomesha watoto wao kwa kuwa Serikali imeendelea kulipa ada kwa
wanafunzi wote kuanzia elimu ya msingi hadi kidato cha sita.
Vilevile, amehimiza wananchi wa
Bugelenga kumchagua mgombea Urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa
katika kipindi cha uongozi wake amekuwa na mapenzi na wananchi hao kwa kutoa
fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Naye, Mgombea wa Udiwani Kata ya
Bugelenga, Donald Rubigisa amewashukuru wananchi wa Kata hiyo kwa kushirikiana
naye katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo kujenga
shule.
Amemshukuru Dkt. Biteko kwa
kusaidia kujenga daraja kubwa lililoondoa adha ya usafiri kwa wananchi hususan
wakati wa masika.
“ Nawashukuru kwa imani yenu
kwangu nataka niwaambia mimi nitafanya kazi, mkinichagua mimi, Dkt. Biteko na
Dkt. Samia Suluhu Hassan tutatekeleza miradi mipya ya maendeleo,” amesema Dkt.
Biteko.
Aidha, amesema Kata yake ina
shule zinazohitaji ukarabati ikiwemo Shule za Msingi Bufanka, Bugelenga na
Msasani hivyo amemuomba Dkt. Biteko mara atakapo chaguliwa tena kuwa mbunge
asaidie kuboresha shule hizo.
Pia, amesema Kata hiyo inahitaji
chumba cha kuhifadhia maiti na kukosa mawasiliano ya simu ya uhakika.
Mgombea huyo amewahimiza wananchi
wake Oktoba 29 kujitokeza kwa wingi na kuwachagua wagombea wa CCM.
0 Maoni