Polisi Mbeya: Kampeni ya usalimishaji silaha kwa hiari kudumu miezi miwili

 

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limetangaza kuanza kwa kampeni maalum ya usalimishaji wa silaha haramu kwa hiari, kampeni itakayodumu kwa kipindi cha miezi miwili kuanzia Septemba 1 hadi Oktoba 31, 2025.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, SACP Benjamin Kuzaga, amesema kampeni hiyo inalenga kuwawezesha wananchi wanaomiliki silaha kinyume cha sheria, kwa kujua au kutokujua, kuzisalimisha bila kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Mwananchi yeyote anayemiliki silaha haramu anatakiwa kusalimisha silaha hiyo kwa hiari katika ofisi za Serikali za Mtaa au Kijiji kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni, au katika kituo chochote cha Polisi kilicho karibu naye,” alisema SACP Kuzaga.

Ameeleza kuwa kwa watakaojitokeza ndani ya muda huo maalum, Jeshi la Polisi halitachukua hatua yoyote ya kisheria, lakini baada ya kumalizika kwa kampeni hiyo, operesheni kali itafanyika kwa lengo la kuwabaini na kuwachukulia hatua wote watakaokaidi agizo hilo.

“Baada ya Oktoba 31, 2025, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya litaanza operesheni maalum na msako mkali dhidi ya wale wote watakaobainika kuendelea kumiliki silaha kinyume cha sheria,” alionya Kamanda huyo.

SACP Kuzaga ametoa rai kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kuhakikisha wanawajulisha wengine kuhusu tangazo hilo, ili kuondoa kisingizio cha kutokufahamu taarifa hiyo pindi muda wa kampeni utakapoisha.

Aidha, amewahimiza wananchi kuwa wazalendo kwa kushiriki kikamilifu katika kampeni hiyo kwa ajili ya kulinda amani na usalama wa jamii.

Chapisha Maoni

0 Maoni