Mradi wa Barabara ya Kyema - Katerelo wafikia asilimia 80

 

Mradi wa Barabara inayowaunganisha wananchi wa kata ya Katerelo  na Kata za Bujugo na Kasharu  Maarufu kama Kyema-Katerelo  unaotekelezwa na Wakala ya Barabara  za mjini na vijijini (TARURA) kwa kiwango Cha Lami kilometa  0.55  chini ya mkandarasi wa ndani  Kashico LTD umefikia asilimia 80.

Meneja wa TARURA wilaya ya Bukoba  Mhandisi Emmanuel Yahana amesema mradi huo umetekeleza kigezo namba 2.2 cha Mwenge wa Uhuru na sera ya barabara na mradi ulianza kutekelezwa Agosti 16 mwaka 2024 ukitarajiwa kukamilika Octoba 2025.

Amesema mradi huo unazisaidia kata hizo kufuata huduma katika Halmashauri ya Bukoba  huku akitaja uwepo wa ongezeko la majengo ya kibiashara katika eneo hilo na kupunguza changamoto ya wananchi kuzunguka kuzifikia kata hizo huku wengine wakitumia gharama nyingi Kufika katika Ofisi za Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Bukoba.

"Mradi huo umetekelezwa kwa  awamu 4 na sasa tunaendelea vizuri ambapo sasa katika hatua zote za utekelezaji ni kumrahisishia mwananchi kupata huduma na katika maeneo haya tumeanza kushuhudia ujenzi wa maduka na ongezeko la wakazi wakati zamani hata barabara ilikuwa haipitiki," alisema Yohana.

Baadhi ya Wananchi wa Kata ya Katerero Halmashari ya Bukoba Mkoani Kagera wameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuwajengea mradi barabara hiyo kwani kwa sasa hawana hofu na vyombo vyao vya Usafiri.

 Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2025  imeweka jiwe la Msingi katika mradi huo ambao unaendelea kutekelezwa kwa viwango huku watumishi wa  jengo jipya La Halmashauri mpya Ya wilaya ya Bukoba wakishuhudia lami hadi mlangoni kwao.

Kiongozi wa mbio za mwenge wa Uhuru kitaifa ndugu Ismail Ussi ameipongeza TARURA kwa usimamizi na utekekezaji barabara na kuwataka wananchi waendelee kutunza miundombinu ya barabara na kufanya uwekezaji kwani uwepo wa barabara unarahisisha Mawasiliano.



Chapisha Maoni

0 Maoni