Waziri Kombo awasili nchini Uingereza kwa ziara rasmi

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahamoud Thabit Kombo, amewasili nchini Uingereza kwa ziara rasmi inayotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 8 hadi 12 Septemba, 2025.

Lengo la ziara hiyo ni kuimarisha uhusiano bora na wa kihistoria kati ya Tanzania na Uingereza.

 Wakati wa ziara hiyo, Mheshimiwa Kombo atamwakilisha Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kama Mgeni Rasmi katika ufunguzi wa kituo kipya cha Masuala ya Kimataifa cha ODI Global utakaofanyika Westminster, London, tarehe 9 Septemba 2025.

Akiwa London, Mheshimiwa Waziri Kombo pia atashiriki katika mfululizo wa vikao vya viongozi waandamizi wa Serikali ya Uingereza, Waziri anayeshughulikia masuala ya Afrika; pamoja na Waziri anayeshughulikia Masuala ya Tabianchi.

Katika hatua nyingine ya kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, Waziri Kombo atakutana na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Mhe. Shirley Ayorkor Botchwey, na Katibu Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Bahari (IMO), Mheshimiwa Arsenio Dominguez.

Aidha Waziri Kombo atafanya vikao na taasisi muhimu za Uingereza za fedha za maendeleo na uwekezaji, ikiwemo British International Investment (BII) na UK Export Finance (UKEF), pamoja na wawakilishi wa King’s Foundation kama juhudi za kuboresha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Uingereza ambao ni msingi mkuu wa sera ya mambo ya nje ya Tanzania.

Ili kuimarisha zaidi ushirikiano wa kiuchumi, Waziri Kombo atashiriki pia katika meza ya majadiliano ya kibiashara na makampuni teule ya Uingereza kwa ajili ya kubaini fursa katika biashara, uwekezaji, nishati safi, miundombinu, na sekta nyingine za kipaumbele.



Chapisha Maoni

0 Maoni