Mpina ateuliwa kugombea urais, ACT-Wazalendo yakataa gari la kampeni la INEC

 

Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Luhaga Mpina, ametangazwa rasmi kuwania nafasi hiyo na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), siku chache kupita baada ya Mahakama Kuu kumrejesha kwenye kinyang’anyiro hicho.

Mpina aliteuliwa rasmi baada ya kuwasilisha fomu zake kwa Mwenyekiti wa INEC, Jaji mstaafu Jacobs Mwambegele, katika ofisi ndogo za tume hiyo jijini Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya zoezi hilo, Jaji Mwambegele alisema Tume imeamua kuwapatia wagombea wote wa urais gari moja kila mmoja, pamoja na dereva, kwa ajili ya kusaidia kampeni zao.

“Tume imeamua kumpatia kila mgombea gari moja pamoja na dereva kwa matumizi ya kampeni, ili kuweka usawa,” alisema Jaji Mwambegele.

Hata hivyo, Chama cha ACT-Wazalendo kimekataa kupokea gari hilo aina ya Toyota Land Cruiser GX VXR lililotolewa na Tume kwa ajili ya kampeni.

Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Omar Shaban, alisimama na kueleza kuwa chama hakitahitaji kutumia rasilimali hiyo.

“Kwanza tunashukuru sana kwa ukarimu mliotuonyesha, lakini tumependelea kutochukua gari. Tupo vizuri na tunaomba rasilimali hiyo isaidie kwenye matumizi mengine,” alisema Shaban.

Akijibu uamuzi huo, Jaji Mwambegele alisema tume haina shinikizo kwa chama chochote kupokea gari hilo, akieleza kuwa lengo lilikuwa ni kuhakikisha usawa katika kipindi cha kampeni.

“Sawa, ni mapenzi yenu. Lengo la magari haya lilikuwa ni kuweka usawa katika kampeni, lakini kama hamtalihitaji, tume italitumia kwa matumizi mengine,” alisema.

Hatua hiyo ya uteuzi wa Mpina inafuatia uamuzi wa Mahakama Kuu wiki hii, uliomrejesha rasmi kwenye mchakato wa uchaguzi baada ya kushinda kesi aliyofungua dhidi ya INEC, akipinga kuenguliwa kwake katika mchakato wa awali wa uteuzi.





Chapisha Maoni

0 Maoni