Mgombea Urais ADC aahidi magari ya kuchimba visima kila Halmashauri

 

Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Wilson Elias Mulumbe, amesema serikali ya ADC itahakikisha kila halmashauri nchini inakuwa na magari ya kisasa ya kuchimba visima ili kuondoa kabisa tatizo la maji safi na salama kwa wananchi.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika leo katika Kata ya Kingolwira, Mtaa wa Bomba la Zambia mkoani Morogoro, Mulumbe amesema tatizo la maji limeendelea kuwa kero kwa wananchi wengi, hasa vijijini, na ni muda sasa hatua madhubuti zichukuliwe kulimaliza.

“Tunataka wananchi wetu waache kuteseka kwa kukosa huduma ya msingi kama maji. Serikali ya ADC itahakikisha kila halmashauri inapata gari la kuchimba visima ili kila mtu apate maji safi na salama,” alisema Mulumbe.

Mbali na sekta ya maji, mgombea huyo ameahidi kuboresha huduma nyingine muhimu za kijamii zikiwemo elimu, afya, nishati na miundombinu ya barabara, akieleza kuwa huduma hizo zitapewa kipaumbele katika mipango ya maendeleo ya ADC.

Katika hatua nyingine, Mulumbe alisema serikali yake itaweka wenyeviti wa serikali za mitaa kote nchini kwenye mfumo rasmi wa malipo kwa kuwalipa mishahara, ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wao mkubwa katika kusimamia maendeleo ya wananchi.

“Wenyeviti wa mitaa ni wawakilishi wa wananchi wa ngazi ya chini kabisa. Tunataka nao watambulike rasmi kwa kazi zao kwa kupewa stahiki kama watumishi wengine wa umma,” alisema.

Mulumbe alisisitiza kuwa chama cha ADC kina dira na mikakati madhubuti ya kuleta maendeleo ya kweli kwa Watanzania wote, kwa kusimamia kwa ufanisi rasilimali za taifa, kuimarisha uwazi katika utawala na kupambana na ubadhirifu wa mali za umma.

Kampeni za uchaguzi mkuu zinaendelea kushika kasi huku wagombea mbalimbali wakiendelea kuwasilisha sera na ahadi zao kwa wananchi. Uchaguzi mkuu unatarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Chapisha Maoni

0 Maoni