WAZIRI
MKUU, Mhe. Kassim Majaliwa amesema kuwa kiwango cha udumavu miongoni mwa watoto
walio chini ya umri wa miaka mitano nchini kimeshuka kutoka asilimia 48 mwaka
1992 hadi asilimia 30 mwaka 2022.
Ameongeza
kuwa, kiwango cha ukondefu miongoni mwa watoto walio chini ya miaka mitano
kimepungua kutoka asilimia 5 mwaka 1992 hadi asilimia 3.2 mwaka 2022.
Amesema
hayo leo Jumanne (Septemba 30, 2025) wakati alipofunga mkutano wa 11 wa wadau
wa lishe nchini, uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa APC uliopo Bunju
Jijini Dar es Salaam.
Amesema
kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
inatambua kuwa lishe si suala la kiafya pekee, bali ni nguzo ya maendeleo ya
rasilimali watu, uchumi na jamii. “Dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kila
Mtanzania anakuwa na chakula cha kutosha, afya njema na lishe bora.”
Kadhalika,
Mhe. Majaliwa amesema kuwa Rais Dkt. Samia ameendelea kuwa kinara wa
mapambano dhidi ya utapiamlo kwa kuhakikisha masuala ya lishe yanapewa
kipaumbele kwa kuimarisha bajeti, kuboresha mifumo ya ufuatiliaji na
uhamasishaji wa afua za lishe kuanzia ngazi ya taifa hadi vijijini.
“Jitihada hizi zilimuwezesha kupata tuzo ya
Global Goalkeeper kutoka Taasisi ya Gates Foundation, kutokana na mchango wake
mkubwa katika kusukuma mbele Malengo ya Maendeleo Endelevu, hususan kwenye afya
ya mama, mtoto na lishe.”
Katika
hatua nyingine, Mhe. Majaliwa amesema kuwa kiwango cha uzito uliozidi na
uzito kupita kiasi (kiribatumbo) hasa miongoni mwa wanawake wa umri wa kuzaa
kimeongezeka kutoka asilimia 28 mwaka 2015 hadi asilimia 37 mwaka 2022.
“Changamoto hii inaakisi mabadiliko ya ulaji na mtindo wa maisha ulioikumba sio
tu Tanzania bali dunia nzima.”
Aidha,
Mhe. Majaliwa ametoa wito kwa Wizara na Taasisi zote za umma na binafsi
kutenge rasilimali za kutosha kwa ajili ya afua za lishe na kuziweka katika
mipango yao ya kila mwaka ili kuongeza uwajibikaji na uendelevu katika
kutekeleza mipango iliyopangwa.
Pia, Waziri Mkuu Majaliwa amezitaka Taasisi za Utafiti na Vyuo vya Elimu ya juu
kuendeleza tafiti katika masuala ya lishe pamoja na kuhakikisha ripoti za
tafiti hizo zinatumika kuboresha sera na mikakati nchini.
Kwa
upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana Ajira na Wenye
Ulemavu) Mhe. Ridhiwan Kikwete amesema kuwa Serikali itahakikisha kuwa wadau wote
walioanishwa katika Mpango Jumuishi wa masuala ya Lishe wanaendela kutekeleza
majukumu yao. "Hii ni pamoja na kuhakikisha kuwa Wizara zote zinaingiza
masuala ya lishe katika mipango ya kibajeti kila mwaka."




0 Maoni