Mgombea
urais wa Chama cha National Liberation for Democracy (NLD), Doyo Hassan Doyo,
ameibua kero tano zinazowakabili wananchi wa Mkoa wa Geita, huku akiahidi
kuzitatua endapo atachaguliwa kuwa Rais katika Uchaguzi Mkuu..
Akihutubia
wananchi katika mikutano ya kampeni iliyofanyika jana Septemba 29, 2025 katika
eneo la Stendi ya Zamani, Jimbo la Sengerema, na baadaye Kata ya Buseresere,
Doyo alisema changamoto hizo zimekuwa ni kilio cha muda mrefu kwa wananchi wa
Geita na maeneo mengine ya Kanda ya Ziwa.
Katika
hotuba yake, Doyo alitaja kero kubwa kuwa ni ubovu wa barabara unaosababisha
gharama kubwa za usafiri kwa wananchi, hali inayochangia ugumu wa maisha na
kudidimiza shughuli za kiuchumi.
“Barabara
mbovu ni adui wa maendeleo. Zinawafanya wananchi walipie gharama kubwa
kufikisha bidhaa sokoni, wagonjwa kushindwa kufika hospitali kwa wakati, na
hata wanafunzi kuchelewa mashuleni. Tutashughulikia hili ndani ya mwaka wa
kwanza,” alisema.
Kero ya pili
aliyoitaja ni ukosefu wa dawa na vifaa tiba katika vituo vya afya vya umma,
akieleza kuwa hali hiyo inahatarisha maisha ya wananchi, hasa wa kipato cha
chini.
“Ni jambo
la kusikitisha kuona mama mjamzito anakwenda kliniki anakosa hata vidonge vya
kuongeza damu. Serikali inapaswa kuwekeza kwenye afya ya watu wake,” aliongeza.
Doyo pia
aliibua changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama, akisema kuwa bado
kuna vijiji na kata nyingi ndani ya Geita ambavyo havina huduma ya uhakika ya
maji, hali inayowaathiri zaidi wanawake na watoto.
Kero
nyingine ni kukosekana kwa masoko yenye tija kwa wakulima, ambapo alisema kuwa
mazao mengi ya wakulima yanaharibika au kuuzwa kwa hasara kutokana na ukosefu
wa miundombinu bora na sera rafiki za masoko.
“Wakulima
wameachwa bila dira. Tutaanzisha mifumo ya uhakika ya masoko, kuongeza thamani
ya mazao na kuhakikisha mkulima anafaidika na jasho lake,” aliahidi.
Doyo
alihitimisha kwa kueleza kuwa endapo wananchi watamchagua, atahakikisha
mikakati iliyopo ndani ya Ilani ya NLD inatekelezwa kwa vitendo, huku akiahidi
kuanza kushughulikia kero hizo tano ndani ya mwaka mmoja wa kwanza madarakani.

0 Maoni