Wakati dunia ikipiga hatua kuelekea kupunguza matumizi ya
nishati inayozalisha hewa ukaa na kuongeza matumizi ya nishati safi, viwanda
vya kusafisha madini ya kinywe (graphite) vya Godmwanga Gems vinaibuka kuwa
tafsiri ya ujenzi wa Tanzania ya viwanda na jinsi madini yanavyochochea ukuaji
wa viwanda Tanzania.
Viwanda hivyo viwili vinavyopatikana katika Vijiji vya
Kwedikabu na Kwamsisi Wilayani Handeni Mkoa wa Tanga, vinamilikiwa na Mtanzania Godlisten Mwanga,
kwa asilimia 100 na kutumia rasilimali za madini za Tanzania, kwa kuchakata na
kugeuza kinywe ghafi kuwa tayari kwa matumizi ya viwandani.
Viwanda hivyo ni vya kwanza nchini Tanzania kuanza
uzalishaji wa madini Kinywe na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya tatu barani
Afrika baada ya Madagascar na Msumbiji na kuhakikishia nafasi ya Tanzania kama
kiungo muhimu katika usambazaji wa bidhaa hiyo muhimu duniani.
Septemba 08, 2025, Akizungumza na Kitengo cha Mawasiliano
Wizara ya Madini, Meneja wa Kiwanda B, Henry Joseph alieleza kuwa, kuanzishwa
kwa viwanda hivyo kumesaidia kuimarisha nafasi ya Tanzania katika uchumi wa
kijani (green economy) kutengeneza ajira kwa wenyeji, utengenezaji na ukarabati
wa miundombinu ya afya, elimu, barabara, ukuaji wa kiuchumi sambamba na
kuonesha jinsi madini yanavyoweza kuwa nguzo muhimu ya ukuaji wa viwanda
nchini.
Uwekezaji wa
Viwandani na Teknolojia
Viwanda vya Godmwanga vina uwezo wa kuchakata na kusafisha
graphite hadi kiwango cha juu cha asilimia 95 kinachokubalika kimataifa. Hatua
inayofanya Tanzania kuwa msambazaji wa malighafi muhimu kwa sekta kama betri za
umeme, vifaa vya kiteknolojia na vilainishi vya viwandani, mashine muhimu na
magari hivyo kuwa sababu ya kuanzishwa kwa viwanda vingine vinavyotegemea
malighafi hizi.
Ajira, Mafunzo, na
Uwezo wa Jamii
Kupitia mafunzo ya kazi, mafunzo ya ufundi, na mpangilio wa
usalama kazini, wakazi wa Kata ya Kwamsisi na vijiji vya jirani wanapata ajira
za moja kwa moja viwandani na ajira zisizo za moja kwa moja kupitia mnyororo wa
thamani (supply chain). Hii inaongeza mapato ya kaya, kuboresha elimu na
kuongeza mahitaji ya huduma za afya na biashara ndogo ndogo. Uwezo huu wa
kibinafsi ulipelekea kuundwa kwa wajasiriamali wadogo waliokuwa wazalishaji wa
vipuri, huduma za usafiri, uchumi na maendeleo endelevu kwa wakazi.
Ushindani wa Kimataifa na Fedha ya Kigeni
Kwa kutoa graphite yenye ubora wa juu, Kampuni Godmwanga
imefanikiwa kuingia katika masoko ya nje, hususani Marekani, China na Korea
Kusini huku ikileta fedha za kigeni. Mapato haya pia yanasaidia Serikali
kuwasilisha Sera za kuendeleza sekta ya madini kwa njia endelevu.
Uendelevu na
Ushirikiano wa Jamii
Viwanda vimetengeneza ajira rasmi zaidi ya 616 wengi wakiwa ni wakazi wa maeneo ya jirani na miradi hiyo. Kampuni ya Godmwanga pia inashirikiana na jamii kupitia Wajibu wa Kampuni kwa Jamii (CSR) kwa kutengeneza na kukarabati miradi ya kijamii kama shule, vituo vya afya na miundombinu ya barabara.
Jinsi Viwanda
Vinavyobadili Maisha ya Wakazi wa Kwamsisi
Subira Hasssan na Hellen David ni miongoni mwa wafanyakazi
wa Kiwanda cha Godmwanga Gems Ltd, wanakiri kuwa uwepo wa mradi huo umesaidia
kuyabadili maisha yao binafsi pamoja na vijiji vya Kwedikabu, Kwamsisi na
maeneo ya jirani kwa kuleta ajira rasmi na zisizo za moja kwa moja. Miradi hii
na mengine katika Wilaya ya Handeni, taratibu imeondoa simulizi maarufu za
Kwamsisi na kuleta taswira mpya ya maendeleo.
Mwanzo wa Taifa Lenye
Viwanda Vinavyosimamiwa na Rasilimali
Simulizi ya Godmwanga ni mfano wa jinsi Kampuni moja inaweza
kuwa kivutio cha mabadiliko: kutoka mgodi mdogo hadi mfululizo wa viwanda
vinavyochangia ukuaji wa taifa. Kwa kuingiza teknolojia, kuwekeza kwa wananchi,
na kushirikiana na Serikali na jamii, madini siyo tu rasilimali ya kuuza bali
vyanzo vya kuendeleza viwanda, kuimarisha uchumi, na kubadilisha mustakabali wa
kizazi kipya.
Kwa mujibu wa Utafiti wa Shirika la Nishati la Kimataifa
(International Energy Agency- IEA) uliofanyika Mei 2025, unaonesha kuwa
mahitaji ya jumla ya Kinywe mnamo 2024 yalikuwa tani milioni 4.8, mahitaji ya
sekta ya teknolojia safi pekee yalifikia tani milioni 1.5. IEA inakadiria
mahitaji ya jumla kufikia tani milioni 8.219 ifikapo mwaka 2030 .
Madini ya Kinywe hutumika kutengeneza betri za magari,
magari ya umeme, vilainishi vya mitambo muhimu, vituo vya utafiti kwa
teknolojia ya nishati, vifaa vya utafiti wa anga na viwanda vya kutengeneza
vifaa vya elektroni na kadhalika.
Godmwanga Gems Ltd inaonesha jinsi madini pale yanapochakatwa kwa ubunifu na kuyaongezea thamani yanavyoweza kuwa kiini cha kuzalisha viwanda, kutengeneza ajira, kuvutia uwekezaji, na kuendeleza miundombinu ya Taifa. Ni mfano wa wazi wa azma ya Tanzania ya viwanda vinavyotokana na rasilimali zake zikiwemo za madini kama Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025-2050 inayoelekeza.
0 Maoni