Mgombea wa Ubunge Jimbo la Bukombe, Ndugu Doto Mashaka
Biteko amewaasa wananchi wa Kata ya Namonge, kujitokeza kwa wingi tarehe 29
Oktoba kumpigia kura Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Rais kwa kuwa ndiye mwenye
nia thabiti ya kuwaletea maendeleo.
Dkt. Biteko amesema hayo leo Septemba 9, 2025 katika mkutano
wake wa kunadi sera kwa wananchi wa Kata ya Namonge wilayani Bukombe mkoani
Geita.
Amesema awali sekta zote katika kata ya hiyo zilikuwa
zikisuasua kimaendeleo ikilinganishwa na maendeleo yaliyofikiwa sasa.
“Kata hii haikuwa na barabara ya kutoka Uyovu - Namonge -
Nyalamandula, haikuwa na zahanati wala shule za kutosha hivyo ilikuwa na
maendeleo duni,” amesema Dkt. Biteko.
Amesema jitihada zilizofanywa na Serikali ya Rais Samia
katika kuwaletea maendeleo wananchi hao ni kutekeleza miradi mbalimbali ya
maendeleo ikiwemo ujenzi wa zahanati na kituo cha afya.
“ Nataka
niwahakikishie mkinichagua tutaongeza wodi na zahanati, tunataka watu wa
Namonge waishi kama Watanzania wa daraja la juu, Tutahakisha tunaongeza shule,
kuna vijiji havikuwa na shule na tumejenga shule mpya. Tumekuja hapa kuomba
kura ili tumchague Rais Samia kwa vile ni kumchagua yeye ni kuchagua
maendeleo,” amesema Dkt. Biteko.
Ameelezea matarajio ya CCM ni kuifanya Kata ya Namonge iwe
kituo cha kilimo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara na hospitali.
Pia, amesema CCM ikipata ridhaa ya kuongoza katika miaka mitano ijayo Serikali itatoa
shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kuwakopesha vijana ili wazitumie kwa kufanya
biashara sambamba na kutoa mikopo kwa wanawake na watu wenyeulemavu.
“Namonge ina wapiga kura zaidi ya 30,000 hivyo nawaomba
Oktoba 29 mwaka huu tujitokeze kwa wingi tukampigie kura Rais Samia. Tunachotaka ni maendeleo na
nataka kuwahakikishia Rais Samia anatupenda mno Bukombe na mwezi Oktoba atakuja
hapa. Heshima pekee tutakayompa Rais
wetu ni kumpigia kura kwa wingi, msiniangushe,” amesisitiza Dkt. Biteko.
Akimnadi mgombea udiwani wa Namonge, Mlalu Bundala amesema
ni mtu makini anayejua shida za wananchi na yuko tayari kuhakikisha Kata hiyo
inapata maendeleo.
Naye, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Geita, Amani
Msuwa amesema kuwa Rais Samia ametekeleza miradi mingi ya maendeleo mkoani humo
hivyo Oktoba 29 wananchi wampigie kura pamoja na mgombea Ubunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto
Biteko.
Mgombea wa Udiwani
Kata ya Namonge, Mlalu Bundala amewashukuru wananchi wa Kata hiyo kwa
kujitokeza kwa wingi katika mkutano huo.
Aidha, amesema katika Kata yake, Rais Samia ametoa fedha kwa ajili ya ujenzi
wa barabara ya km 61, mtandao wa maji Namonge wenye mita za ujazo 21, shule za
msingi 7, shule za sekondari 3 pamoja na kituo cha afya.
Ameongeza kuwa Kata hiyo ina mtandao wa umeme katika vijiji
vyote na jitihada za kufikisha umeme kwenye vitongoji zinaendelea.
0 Maoni