Uwanja wa Ndege wa kisasa unaotarajiwa kukamilika Oktoba
mwaka huu, ni miongoni mwa uwekezaji wa kimageuzi unaoendelea kufanywa na
Serikali kuifungua sekta adhimu ya utalii.
Akishuhudia kuendelea kukamilika kwa Uwanja wa Ndege wa
kisasa unaojengwa kwenye eneo la Mtemere kwenye Hifadhi ya Taifa ya Nyerere,
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, amesema
uwanja huo utafungua “Serengeti” mpya hapa nchini ambayo ni Hifadhi ya Nyerere.
“Hifadhi hii ipo dakika 35 kwa ndege kutoka Dar lakini inaunganishwa
na Barabara kadhaa ikiwemo ile ya Kisarawe-kutokea Dar es Salaam; Bigwa-Kisaki
kama mtu anatokea Morogoro lakini pia inayopitiwa na treni ya Tazara kwa
stesheni ya Vuga.”
“Uwanja huu utakaokuwa na urefu wa km 1.8 kwa ile barabara
ya ndege pekee lakini na barabara nyingine za akiba pia utakuwa na chumba cha
kisasa cha kuongozea ndege, majengo ya kuondoka na kuwasili abiri yenye huduma
za kisasa, ofisi na maegesho ya magari,” alisema Dkt. Abbasi akiwahimiza
wakandarasi kuhakikisha mwezi ujao tabaka gumu la kwenye njia ya kuruka na
kutua ndege kukamilika.
Utalii umeongezeka kwa kiasi kikubwa katika Hifadhi ya
Nyerere kutoka wastani wa watalii 15,000 tu kwa mwaka 2021 hadi watalii 47,000
mwaka jana 2024.
Ikishinda Tuzo ya Eneo Lenye Mwonekano Munawari Afrika (Africa’s Leading Scenic National Park 2025) wakati wa Tuto za Utalii za Dunia-Kanda ya Afrika na Bahari ya Hindi, Hifadhi ya Nyerere inazidi kufahamika kwa mandhari zake adhimu, makumi ya wanyama, mito kama Mto Rufiji na sehemu kubwa chini ya Mto ikitengeneza maziwa mengi yanayotokana na mienendo ya kijiografia lakini eneo la juu likiwa na bwawa kubwa lenye upana wa km 30 na urefu wa km 100; sehemu ya Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Mwalimu Nyerere.
0 Maoni