KATIBU
wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama
Cha Mapinduzi, Kenani Laban Kihongosi amesema Halmashauri Kuu ya CCM
ya Taifa (HKT) imefanya kikao chake cha kawaida jijini Dodoma chini
ya Mwenyekiti wake, Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya
Kihongosi iliyotolewa leo Alhamisi Mei 7, 2026, pamoja na mambo
mengine Halmashauri Kuu ilifanya tathmini ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka
2025 na kujadili hali ya kisiasa nchini.
Amesema katika kikao
hicho, Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa ilimshukuru na kumpongeza
Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.
Samia Suluhu Hassan, kwa kuunda Tume ya Rais ya kuchunguza matukio
yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Pia,
Halmashauri Kuu imeipongeza Tume ya Uchunguzi iliyoongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman kwa kufanya kazi yake kwa weledi, uadilifu na
kwa kuzingatia misingi ya sheria za nchi na za kimataifa. Aidha,
imeipongeza Serikali kwa hatua zilizoanza na zitakazoendelea
kuchukuliwa katika kutekeleza mapendekezo yote yaliyotolewa na tume
hiyo.
Katika hatua nyingine, Halmashauri Kuu kwa kauli moja
imevipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kazi kubwa ya kulinda
nchi na kuhakikisha hali ya amani na utulivu inarejea haraka katika
maeneo yote ya nchi mara baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Vilevile, kikao hicho kimeunga mkono pendekezo la Kamati Kuu kutoka kikao chake cha Aprili 28 hadi 29, 2026 la kufanya tathmini ya kina ya CCM kwa lengo la kukiimarisha na kuchukua hatua thabiti za kukiboresha kimuundo, kiutendaji na kiuchumi.
#MezaYaUmoja

0 Maoni