Tume Huru
ya Uchaguzi (INEC) imekitaka Chama cha ACT Wazalendo kuzingatia masharti ya
Kanuni ya 35 ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za mwaka 2025, inayohusu
utaratibu na ratiba za ubunge, ili kuhakikisha mchakato wa uchaguzi unaendeshwa
kwa mujibu wa sheria na miongozo iliyowekwa.
Kauli
hiyo ya INEC imekuja kufuatia taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti rasmi ya ACT
Wazalendo tarehe 21 Septemba 2025, ikieleza kuwa kutakuwa na uzinduzi wa Ilani
ya Uchaguzi wa chama hicho katika Makao Makuu ya chama, tukio litakalofuatiwa
na uzinduzi wa kampeni za ubunge katika Jimbo la Segerea.
Taarifa
hiyo ya chama pia ilieleza kuwa shughuli hizo mbili zitahudhuriwa na waliotajwa
kuwa ni wagombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kupitia ACT Wazalendo, ambao ni Ndugu Luhanga Joelson Mpina na Ndugu
Fatma Abdulhabib Ferej.
Hata
hivyo, INEC kupitia taarifa rasmi iliyotolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi,
Kailima Ramadhani Kailima, imeweka wazi kuwa kwa mujibu wa uamuzi wake wa
tarehe 15 Septemba 2025, ACT Wazalendo haina mgombea wa kiti cha Rais wala
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka
huu, baada ya kutengua rasmi uteuzi wa Ndugu Luhanga Joelson Mpina.
0 Maoni