CHAUMMA: Tutarekebisha tofauti za mazingira ya kazi kwa watumishi wa umma

 

Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) kimeahidi kushughulikia tofauti kubwa za mazingira ya kazi kwa watumishi wa umma nchini endapo kitapewa ridhaa ya kuongoza Serikali katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.

Ahadi hiyo imetolewa jana na mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama hicho, Salum Mwalimu, wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika katika Kata ya Majimoto, Wilaya ya Mpimbwe, mkoani Katavi.

Akihutubia mamia ya wananchi waliojitokeza kumsikiliza, Mwalimu amesema kuwa moja ya kipaumbele cha Serikali atakayoiongoza ni kuhakikisha kuwa watumishi wa umma wanalipwa mshahara wa chini usiopungua Sh 800,000 kwa mwezi, baada ya makato, ili kuwawezesha kuishi kwa heshima na kujikimu katika mazingira yoyote wanayofanyia kazi.

“Tunataka mtumishi wa umma popote alipo mjini au kijijini ajisikie thamani ya utumishi wake. Haiwezekani mtumishi wa kijijini mwenye changamoto nyingi apokee mshahara sawa na yule wa mjini pasipo kuzingatia mazingira yao ya kazi,” alisema Mwalimu.

Amesisitiza kuwa watumishi wengi wa umma wanaohamishiwa maeneo ya pembezoni hukumbwa na hali ngumu ya maisha, huku wengine wakihisi kama wameadhibiwa, jambo ambalo amesema litakomeshwa mara moja iwapo CHAUMMA kitashinda.

“Tunataka kujenga mfumo wa ajira wa haki na wa kutia moyo. Mtumishi wa umma anatakiwa afurahie kulitumikia taifa, si kuhisi kama ameachwa au kutelekezwa kwa sababu ya mahali alipopelekwa,” aliongeza.

Katika hotuba yake, Salum Mwalimu pia aliwataka watumishi wa umma na wananchi kwa ujumla kuendelea kuwa na matumaini, akisisitiza kuwa CHAUMMA inatambua changamoto nyingi zinazoikabili sekta ya utumishi wa umma, hasa maeneo ya vijijini, na kwamba chama hicho kina sera mahususi za kuzitatua kwa njia ya kudumu.

Ahadi hiyo imepokelewa kwa hisia mseto kutoka kwa wananchi waliokuwa uwanjani, ambapo baadhi yao wameeleza matumaini kwamba sera hizo zikitekelezwa zinaweza kubadilisha hali ya maisha ya watumishi wengi walioko maeneo ya mbali.

CHAUMMA ni miongoni mwa vyama vinavyoshiriki uchaguzi mkuu wa mwaka huu kwa mara ya tatu tangu kimesajiliwa rasmi mwaka 2015, na kimekuwa kikisisitiza ajenda za usawa wa kijamii, haki katika ajira na maboresho ya maslahi ya wafanyakazi.

Chapisha Maoni

0 Maoni