Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kinawagombea
bora na imara wenye uwezo wa kuendelea kuleta maendeleo nchini.
Amesema kuwa safu hiyo inaongozwa na mgombea wa Urais wa CCM
Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye katika kipindi chake kinachoishia amefanya
mambo mengi na makubwa ambayo yamewanufaisha na kugusa maisha ya kila siku ya
watanzania.
Amesema hayo leo Jumapili (Septemba 14, 2025) wakati wa
Uzinduzi wa Kampeni za ubunge wa jimbo la Lindi Mjini zilizofanyika katika
viwanja vya shule ya msingi Mnazi Mmoja mkoani Lindi.
“Rais Dkt. Samia amefanya kazi kubwa nchini ikiwemo katika
mkoa wetu wa Lindi, hatuwezi pata mafanikio kama hatuwezi kuwa na muendelezo wa
uongozi, Rais huyu ameleta fedha za miradi, upo umuhimu wa kumuongezea muda ili
yale aliyoyaanza ayaendeleze, tunamuachaje Rais Dkt. Samia? kwanini tumuache?”
alihoji Mheshimiwa Majaliwa.
Ameongeza kuwa watanzania hawana sababu ya kuwa na mashaka
na Rais Dkt. Samia kutokana na kazi kubwa aliyoifanya katika kipindi kifupi cha
uongozi wake kwenye sekta za elimu, afya, kilimo, miundombinu. “Ilani hii
imeongeza mambo mengine mazuri kwa ajili ya Wana-Lindi, msifanye makosa Oktoba 29 mwaka huu.”
Akimuombea kura mgombea ubunge wa jimbo hilo, Mohamed Utaly,
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Mheshimiwa Utaly ni mgombea imara ambaye
amethibitisha hayo kwa nyakati tofauti hivyo kumpa ridhaa kutaliwezesha jimbo
hilo kuendelea kupaa kimaendeleo.
Naye, Mgombea ubunge huyo Mohamed Utaly amesema kuwa ameamua
kugombea ubunge wa jimbo hilo ili naye aweze kutoa mchango wa kimaendeleo
katika jimbo hilo. “Nilijitayarisha kwa ajili ya kuwatumikia, ninataka tuwashe
tochi ya maendeleo katika jimbo letu, mchagueni Rais Dkt. Samia, wabunge na
madiwani, kapigeni kura za heshima.”
Utaly ameongeza kuwa katika kipindi chake, atawapa uwakilishi makini bungeni pamoja na maeneo mengine atakayotakiwa kufanya hivyo. “Nitatumia taaluma yangu kuhakikisha jimbo letu la Lindi linasonga mbele.”
0 Maoni