Walimbwende 24 wanaoshiriki mashindano
ya Miss Grand Tanzania 2025 kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara, wamefanya
ziara ya siku moja katika Hifadhi ya Pande iliyopo jijini Dar es Salaam tarehe
13 Agosti 2025 kwa lengo la kujifunza masuala ya uhifadhi na utalii wa ndani.
Ziara hiyo iliandaliwa kwa ushirikiano
kati ya waandaaji wa Miss Grand Tanzania na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori
Tanzania (TAWA), ikiwa ni sehemu ya kuwawezesha walimbwende hao kujifunza
masuala ya uhifadhi na utalii na kuwa mabalozi wa vivutio vya utalii wa ndani,
hususan Hifadhi ya Pande.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo,
Kaimu Kamanda wa Hifadhi ya Pande, PC Suleiman Keraryo, alisema hifadhi hiyo ni
kivutio cha kipekee kilichopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam, ambapo wageni
hupata fursa ya kutalii na kujionea vivutio mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujifunza kuhusu historia
ya hifadhi hiyo, bioanuwai na mchango wake katika uhifadhi wa mazingira na
viumbe hai.
“Karibuni sana katika Hifadhi yetu ya
Pande, hifadhi iliyo katikati ya Jiji la Dar es Salaam, ikiwa na wanyamapori wa
aina mbalimbali na vivutio vingine lukuki. Hapa ni mahali sahihi kwenu kujifunza
na kujionea rasilimali za nchi yenu,” alisema Keraryo.
Aidha, alibainisha kuwa mshindi wa
Miss Grand Tanzania 2025 atateuliwa kuwa Balozi wa Hifadhi ya Pande, ambapo
atashirikiana na TAWA katika juhudi za kuitangaza hifadhi hiyo pamoja na
kuchochea utalii wa ndani, sambamba na kuunga mkono juhudi za Serikali katika
sekta ya maliasili na utalii.
Mashindano ya fainali ya Miss Grand
Tanzania yanatarajiwa kufanyika tarehe 16 Agosti 2025 katika Ukumbi wa
Superdome, Masaki – Dar es Salaam.
Uongozi wa Hifadhi ya Pande pia
umeeleza dhamira yake ya kuendeleza ushirikiano na waandaaji wa Miss Grand
Tanzania kwa kuhakikisha kuwa walimbwende wanapata fursa ya kulala ndani ya
hifadhi hiyo na kufanya mazoezi katika mazingira ya asili, ili kuongeza uelewa
wao kuhusu uhifadhi wa mazingira.
Kwa upande wao, walimbwende wameeleza
kufurahishwa na ziara hiyo, hususan kupata fursa ya kuona kwa ukaribu aina
mbalimbali za wanyamapori waliopo hifadhini humo, sambamba na mapokezi mazuri
kutoka kwa maofisa wa TAWA. Pia waliahidi kuwa mabalozi wa kuitangaza hifadhi
hiyo kwa jamii.
Ziara hiyo imeelezwa kuwa ni mwanzo wa ushirikiano endelevu kati ya TAWA na taasisi za kijamii, hususan zinazowalenga vijana, kwa lengo la kuongeza uelewa juu ya umuhimu wa kulinda mazingira na kuendeleza utalii wa ndani kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Na. Beatus Maganja - Dar es Salaam
0 Maoni