Baadhi ya wananchi katika halmashauri
ya wilaya ya Mbarali mkoa wa Mbeya wameipa pongezi wizara ya Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi kwa kuandaa Klinik ya Maalum ya Ardhi kwa ajili ya kuongeza
kasi ya umlikishaji ardhi katika maeneo yao.
Klinik Maalum ya Ardhi katika
halmashauri ya wilaya ya Mbarali imeanza tarehe 6 Agosti 2025 na inatarajiwa
kumalizika tarehe 18 Agosti 2025 na inahusisha viwanja 30,700 vilivyopangwa na
kupimwa kupitia Mradi wa Uboreshaji wa Usalama wa Milki (LTIP). Mradi huo
ulifanyika katika Kata ya Rujewa, Ubaruku, Lugelele, Mabadaga, Igulusi,
Kongoromswiswi na Madibira.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti
tarehe 14 Agosti 2025 wakati wa Klinik Maalum ya ardhi ilinayofanyika kijiji
cha Ubaruku wilayani Mbarali, wananchi hao wamesema uamuzi wa wizara ya ardhi
kuandaa klinik hiyo ya ardhi umewarahisishia kupata hati milki za maeneo bila
ya usumbufu.
‘’Hili walilofanya wizara kuandaa
klinik Maalum ya Ardhi katika eneo hili la Mbarali kwa kweli limetufurahisiha
sana kwa kuwa tumepata hati hap hapa, tumesubiri kwa muda mrefu kupata hati na
hatimaye kilio chetu kimesikilizwa’’ amesema Juma Omar mkazi wa Ubaruku.
Kwa mujibu wa wakazi hao wa Ubaruku,
maeneo yao waliwekewa mawe kwa muda mrefu lakini umilikishaji haukufanyika kwa
wakati jambo lililowafanya wananchi kuwa na mashaka juu ya zoezi la
umilikishaji.
Wamesema kuwa, iwapo kasi ya
umilikishaji inayofanyika hasa kwenye maeneo yaliyoainishwa basi wananchi wa
maeneo husika wataweza kunufaika na umiliki wa ardhi yao kwa kupatiwa hati
milki inayoweza kutumika kwa shughuli mbalimbali ikiwemo kukopea katika taasisi
za fedha.
Sheikh Haroun Mkanyanga, mkazi wa
Igawa mbali na kuipongeza wizara ya Ardhi kwa kuandaa Klinik Maalum amewataka
wananchi wa Mbarali kuchangamkia zoezi hilo kwa kuwa limewarahisishia kazi ya
kufuata huduma hiyo ya ardhi umbali mrefu.
‘’Niwatake wamiliki wenzangu wa ardhi
kujitokeza kwa wingi kupata huduma hii ya ardhi hususan hati milki kwa kuwa
ardhi ni kila kitu na unapokuwa na umiliki utaepukana na migogoro ya ardhi kama
vile migogoro ya mipaka’’ amesema.
Kwa upande wake Mratibu wa Program ya
Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi (KKK) Elia Kamihanda amewataka wananchi wa
Wilaya ya Mbarali kujitokeza kwa wingi kupata huduma kupitia zoezi hilo
lililoanza tarehe 6 Agosti 2025 na kuhitimishwa tarehe 18 Agosti 2025 kwa kuwa
huduma zimesogezwa karibu na wananchi.
‘’Niwaombe ndugu zangu wa Mbarali
kuchangamkia zoezi hili kwa kuwa limewasogeza huduma lakini mbali na hapa
watalazimika kufuata huduma katika ofisi zetu jambo ninaloona halileti afya
wakati huduma kwa sasa zipo hapa,’’ amesema Kamihanda.
Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi imeanzisha Klinik Maalum ya Ardhi kwa ajili ya kuongeza kasi ya
umilikishaji ardhi kwenye maeneo ambayo mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki (LTIP)
umetekelezwa.
Klinik hiyo maalum ya ardhi inafanyika
Dar es Salaam katika manispaa ya Ilala, Dodoma eneo la Mpunguzi, Mbeya
halmashauri ya Mbarali na mkoa wa Shinyanga katika halmashauri ya Kahama pamoja
na Manispaa ya Shinyanga.
Kupitia klinik hiyo huduma mbalimbali
zitatolewa kama vile umilikishaji ardhi wa papo kwa hapo kwa wamiliki
waliokamilisha taratibu za umiliki, utoaji elimu kwa wananchi kuhusu matumizi
ya mfumo wa utoaji huduma za ardhi kidigiti (e-Ardhi) na Usaidizi wa ufunguaji
wa akaunti ya Mwananchi kwenye mfumo wa e-Ardhi.
Huduma nyingine ni Uhakiki na utambuzi
wa viwanja vya Wananchi Uwandani, Utoaji wa namba ya malipo (control number) za
ada mbalimbali za Serikali kwa ajili ya umilikishaji pamoja na Upokeaji,
usikilizaji na utatuzi wa migogoro kiutawala.
Wananchi wakisubiri kupatiwa huduma
wakati wa Klinik Maalum ya Ardhi inayoendelea katika Halmashauri ya wilaya ya
Mbarali mkoa wa mbeya.
Baadhi ya watumishi wa wizara ya ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi wakitoa huduma wakati wa Klinik Maalum ya Ardhi wilayani Mbarali mkoa wa Mbeya. Picha na Habari na Munir Shemweta - WANMM - Mbarali.
0 Maoni